
Dar es Salaam. Ili kuharakisha ujumuishaji wa kifedha kwa wanawake, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetaja maeneo ambayo yanapaswa kuwekewa mkazo zaidi ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwao.
Maeneo mengine ni elimu ya kifedha na uwezeshaji, kuwepo kwa sera na utetezi hasa zinazochochea usawa wa kijinsia katika sekta ya kifedha.
Hayo yamesemwa na Naibu Gavana wa BOT, Sauda Msemo wakati akitoa hotuba katika maadhimisho ya siku ya wanawake katika sekta ya fedha yaliyofanyika leo Jumatano, Aprili 9, 2025 yakiandaliwa na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), ambapo pamoja na mambo mengine ulijadili namna ya kuongeza ujumuishaji wanawake katika huduma za kifedha.
Msemo amesema biashara zinazohudumiwa na wanawake ni kati ya zinazokuwa kwa haraka lakini mara nyingi zinashindwa kupata mtaji wanaohitaji.
“Wakati tunaendelea kuunda bidhaa maalumu za benki kwa wanawake, tunahimizwa kuchunguza fursa za kupunguza hatari zinazopatikana kimataifa lakini pia ndani ya nchi. Hii itasaidia kupanua mikopo, upatikanaji wa mtaji kwa wanawake, pamoja na wanajamii wengine,” amesema Msemo.
Eneo lingine ni utoaji wa elimu ya kifedha na uwezeshaji kwani ili kuwezesha wanawake kifedha, upo uhitaji wa kuwekeza katika programu za masilahi ya kifedha zinazowapa wanawake maarifa na ujuzi wa kujiendesha katika mfumo wa kifedha kwa ujasiri.
“Juhudi kama hizi ambazo tayari zipo ndani ya sekta ni kama Nikofit, zinaongeza uelewa kwa jamii lakini zaidi kwa wanawake. Hili ni kuhakikisha kwamba angalau wanapojaribu kupata huduma za kifedha, wanapata kutoka kwa watoa huduma sahihi na pia wawe makini na masharti wanayoyatoa,” amesema.
Eneo lingine ni kuhusu sera huku akisema ni wakati wa kuunda sera zinazochochea usawa wa kijinsia katika sekta ya kifedha, ambayo itasaidia kuwa na usawa mzuri katika usimamizi wa juu na pia ngazi za bodi kwa wanawake na wanaume.
Katika eneo la usawa wa kijinsia, Msemo amesema mwaka jana ulifanyika utafiti ambapo matokeo yake yalionyesha, upo uhitaji wa benki na taasisi za kifedha zote kuzingatia na kushughulikia tofauti za kijinsia katika maeneo yao.
“Ili kufikia usawa wa kijinsia, benki na taasisi za kifedha lazima ziboreshe sera zao za utawala, kuhakikisha angalau theluthi moja ya wajumbe wa bodi ni wanawake. Hii pia inahusisha kurekebisha muundo wa bodi na vigezo vya ufanisi wa wakurugenzi, kuingiza utofauti wa kijinsia katika mipango ya urithi na kuunda mfumo wa wanawake wa kuteuliwa katika nafasi hizo,” amesema.
Amesema kama BoT inazihimiza benki kubadilisha katiba za bodi zao ili kuzingatia nafasi za uongozi za wanawake, kwani hilo ni jambo linaloendana na lengo la kukuza ukuaji wa kiuchumi wa pamoja.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa TBA, Geoffrey Mchangila amesema ujumuishi wa kifedha siyo tu kuhusu upatikanaji bali unahusisha kutengeneza mazingira mazuri ambapo wanawake wanaweza kustawi wakiwa na rasilimali, elimu, na msaada.
“Lazima tuende mbali zaidi ya upatikanaji na tuingie katika uwezeshaji wa kifedha kwa kubuni huduma zetu, kukuza ufadhili wa ushauri na kuhakikisha elimu ya kifedha inapatikana kwa wanawake wote,” amesema
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Erick Massinda amesema taasisi za kifedha ni vyema kuangalia namna ambavyo zinaweza kusaidia wanawake kuwa na hali bora ya kifedha, kujenga usalama wa kifedha zaidi kupitia akiba ya uzalishaji na uwekezaji na wanavyoweza kujenga uhimilivu zaidi kwa wanawake katika kukabiliana na matatizo, kama vile magonjwa, mabadiliko ya tabianchi au mengineyo.