
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu anadaiwa kushirikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma muda mchache baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mbinga mkoani humo.
Bado haijafahamika chanzo cha Lissu, pamoja na walinzi wake wawili, kada mmoja wa chama aliyefahamika kama Shija Shebeshi kushikiliwa na polisi, baada ya kutoa vurumai baina ya wananchi na jeshi hilo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya ameliambia Mwananchi leo Jumatano Aprili 9,2025 kuwa yupo katika ufuatiliaji kuthibitisha kuwepo kwa taarifa hiyo.
“Na mimi ndio nafuatilia hiyo taarifa, bado sijaipata rasmi. Kukiwa na taarifa kamili tutaitoa kesho,” amesema Kamanda Chilya alipoulizwa na Mwananchi kwa simu.
Awali, akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amedai Lissu amekamatwa muda mfupi baada ya kushuka jukwaani, alipomaliza kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mbinga Sokoni.
“Bado hatujui chanzo ni nini? Tumefanya mkutano wa amani na utulivu, ulimalizika polisi walinga’ng’ania kuondoka na Lissu. Licha ya kuanza harambee ya ‘Tone tone’ bado polisi waliendelea kumfuata Lissu.
“Hata hivyo wananchi waligoma Lissu kukamatwa, wakasema mwenyekiti haendi popote ndipo polisi walipoamua kupiga mabomu ya machozi mfululizo ili kuwatawanya na kumchukua mwenyekiti kilazima,” amedai Rupia.
Lissu na viongozi wengine akiwemo makamu mwenyekiti wa chama hicho, bara John Heche wapo kanda ya kusini kunadi ajenda ya ‘No Reforms, No Election’ wakishinikiza Serikali kufanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi ili uwe haki kwa vyama vyote.
Ziara hiyo katika mikoa ya Kusini inayoundwa na Lindi, Mtwara na Ruvuma ilianza Aprili 4, 2025 na inatarajiwa kuhitimishwa kesho Alhamisi kwa mkutano wa hadhara Songea Mjini.
Endelea kufuatilia Mwananchi