
Arusha. Mwili wa mwanaume mmoja ambaye hajafahamika jina wala makazi yake umekutwa pembezoni mwa mto Sekei jijini Arusha, huku ukiwa umeanza kuharibika.
Mwili huo umebainika usiku wa kuamkia leo Aprili 9, 2025 na watoto waliokuwa wanatafuta mbwa wao aliyekimbilia mtoni ambapo inadhaniwa alikuwa anafuata harufu ya mwili huo.
Kubainika kwa mwili huo kunafanya jumla ya matukio ya miili kukutwa mitaani jijini Arusha kufikia manne ndani ya siku 20.
Tukio la kwanza lilitokea machi 26,2025 ambapo miili ya watu wawili wa jinsi ya kike na kiume ilikutwa ikiwa imefukiwa ardhini katika eneo la Muriet jijini hapa ikiwa na majeraha mbalimbali na kutobolewa macho.
Tukio la pili lilitokea asubuhi ya kuamkia Aprili 5,2025 ambapo mwili wa mwanaume ulikutwa katika eneo hilohilo ukiwa pembezoni ya barabara. Mwili huo ulikuwa na majeraha mgongoni.
Akizungumzia tukio la leo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salvas Makweli amesema kuwa jeshi hilo limeanza uchunguzi wa tukio hilo.
“Uchunguzi wa hilo tukio unaendelea na ukikamilika tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari,” amesema Makweli kwa njia ya simu na kukata.
Wakizungumza katika eneo la tukio shuhuda, Pinieli Maiko amesema kuwa wadogo zake wakiwa wanacheza pembeni ya mashamba penye miti ya mapera walionekana kushuka na njia ya mtoni majira ya jioni kabla ya muda kidogo kupanda wakidai kuna mtu amelala pembezoni mwa mto.
“Nilitaka wanionyeshe alipo na nilifuata njia hiyo ambayo mara nyingi watu huwa hawapiti sana na kadri ninavyozidi kushuka nilikuwa napokelewa na harufu kali, nilipokaribia nikaona mkono wa mtu kwa mbali”;
“Sikuweza kuendelea kusogelea nilirudi nyuma na kumwambia mama mmoja jirani yetu kuna mtu kafia mtoni na yeye kuwaambia madereva bodaboda waliokuwa kijiweni, tukashuka wote na kushuhudia mwili wa mtu huyo ukiwa umeharibika vibaya na unatoa wadudu sehemu za mdomoni na puani,”
Naye Eliza Elia amesema kuwa waliona watu wengi wanashuka mtoni na yeye kuamua kufuata nyayo zao na kukuta mwili huo umekaa kwa kuegemea mgomba, huku pembeni yake kukiwa na begi la mgongoni, simu pamoja na chaja.
“Mwili wa mtu huyu mwenye umri mkubwa kidogo huku akiwa na nywele kama kalasinga anaonekana amekufa kwa zaidi ya siku tatu au nne kutokana na kuvimba sana na ilianza kuharibika,” amesema.
Hata hivyo amesema kuwa kwa mtizamo na mashuhuda wenzake mtu huyo si wa maeneo hayo kwani hakuna aliyemtambua.
Mwingine auawa kwa
kukatwa na panga
Katika tukio lingine, Hassan Nakimbetwa (28) mkazi wa Banda Mbili kata ya Sombetini jijini Arusha amefariki dunia baada ya kujeruhiwa na panga kichwani na kusababisha kuvuja damu nyingi.
Akizungumza tukio hilo Kamanda Makweli amesema kuwa atalifuatilia tukio hilo.
“Hilo tukio naomba muda tulifuatilie kujua ukweli na undani wake” amesema Kamanda Makweli.
Mdogo wa marehemu, Elia Nakimbetwa amedai kuwa siku ya tukio Aprili 5, 2025 kaka yake aliletwa nyumbani usiku saa tatu na dereva bodaboda aliyedai ni msamaria mwema aliyemsaidia huku mavazi yake yakiwa yamelowa damu.
“Huyo dereva bodaboda alisema kaka yangu amejeruhiwa eneo la duka na simenti kata hii ya Sombetini na watu wasiojulikana ambao wamekimbia baada ya kutekeleza tukio hilo la kumjeruhi”.
Amesema kuwa kaka yake alikuwa anafanya biashara ya studio ya kuweka muziki na sinema mbalimbali kwenye flashi na CD, lakini pia alikuwa anajishughulisha na muziki wa Bongofleva katika matukio mbalimbali jijini Arusha.
Mama mdogo wa marehemu, Tatu Rajabu amedai kuwa mwanaye amepata ajali hiyo ya kujeruhiwa na mapanga kichwani na watu wanaodaiwa ni wezi waliotaka kumwibia.
“Watu wanasema alijeruhiwa na watu waliotaka kumuibia na katika kupigana nao ndio wakamkata na panga kichwani sehemu ya kichogoni na kusababisha kuvuja damu nyingi sana na kabla ya siku ya tatu kufariki dunia akipatiwa matibabu”.
Amesema kuwa mwanaye baada ya kuletwa na msamaria mwema aliyemfahamu kwao walimpeleka Hospitali ya Oljoro kupata matibabu ikiwa ni pamoja na kushonwa jeraha lake, kisha kupewa dawa na kurudi nyumbani Jumatatu lakini hali haikuwa nzuri hadi alipozidiwa jana Aprili 8,2025 na kumuwahisha Hospitali ya Mount Meru lakini alifariki akiwa njiani.