
Dar es Salaam. Benchi la ufundi la Simba limeamua kumuanzisha mshambuliaji Steven Mukwala katika mchezo wake wa marudiano ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mukwala anaanza badala ya Lionel Ateba ambaye mchezo uliopita ugenini alikuwa katika kikosi cha kwanza.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids amefanya badiliko moja tu leo katika kikosi chake ambalo ni hilo la Mukwala badala ya Ateba lakini ameamua kupanga wachezaji wengine 10 walioanza katika mechi ya mchezo uliopita ambao Simba ilipoteza kwa mabao 2-0.
Uamuzi wa kumpanga Mukwala unaonekana kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na presha ambayo benchi la ufundi la Simba lilipata baada ya mchezo wa kwanza kutokana na kiwango kisichoridhisha ambacho Ateba alikionyesha.
Katika mchezo uliopita, Ateba alionekana kupoteza nafasi nyingi ambazo alipata ndani ya eneo la hatari na haikushangaza kuona mtandao unaojishughulisha na utoaji na utunzaji wa takwimu za soka wa www.fotmob.com ukimuweka mshambuliaji huyo kutoka Cameroon katika nafasi ya pili kwenye kundi la wachezaji waliofanya vibaya zaidi katika mechi hiyo kwa kumpa alama 5.7 kati ya 10 huku kipa wa Simba, Mousa Camara akitajwa kuwa ndiye aliyefanya vibaya zaidi ambapo alipewa alama 4.3.
Kwenye Ligi Kuu nako, Ateba katika mechi 17 alizocheza amefanikiwa kufunga mabao nane akitoa pasi tatu za mabao akitumia dakika 1,176.
Mukwala naye ndani ya mechi 20 alizocheza akiwa ameanza kwenye michezo michache, amefunga mabao tisa akiwa na pasi mbili za mwisho akitumia dakika 736 pekee kutengeneza namba hizo.
Kikosi cha Simba kinachoanza leo kinaundwa na Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Abdulrazack Hamza, Chamou Karaboue, Yusuph Kagoma, Kibu Denis, Fabrice Ngoma, Steven Mukwala, Charles Ahoua na Elie Mpanzu.
Katika benchi kutakuwa na Ally Salim, David Kameta, Valentine Nouma, Edwin Balua, Ladack Chasambi, Debora Fernandes, Awesu Awesu, Joshua Mutale na Lionel Ateba.