
Al Ahly na Mamelodi Sundowns jana zimeweza kuzidhibiti Al Hilal na Esperance kupata ushindi dhidi yao katika mechi za marudiano za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilizochezwa Libya na Tunisia, matokeo ambayo yamezivusha kwenda hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.
Katika Uwanja wa Cheikha Ould Boïdiya jijini Nouakchott, Mauritania, Al Ahly imewaduwaza wenyeji wao Al Hilal baada ya kuwachapa kwa bao 1-0, matokeo ambayo yameifanya Al Ahly isonge mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-0.
Bao pekee ambalo limeihakikishia ushindi Al Ahly jana, limefungwa katika dakika ya 80 na kiungo Emam Ashour.
Nchini Tunisia katika Uwanja wa Olympique Hammadi-Agrebi jijini Radès, Mamelodi Sundowns imelazimisha sare tasa dhidi ya wenyeji wao, Esperance, matokeo ambayo yameivusha timu hiyo ya Afrika Kusini kwenda nusu fainali, ikibebwa na ushindi wa bao 1-0 ilioupata katika mechi ya kwanza wiki iliyopita.
Kwingineko katika mji wa Meknes, Morocco, Pyramids ya Misri imefanikiwa kusonga mbele licha ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa wenyeji wao, FAR Rabat.
Mabao ya Youssef Alfahli na Joel Beya hayakutosha kuifanya FAR Rabat kuitupa nje Pyramids FC ambayo imefaidika na ushindi wa mabao 4-1 ambao iliupata katika mechi ya kwanza ambayo ilikuwa nyumbani.
Hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakamilika leo kwa mchezo utakaozikutanisha Orlando Pirates na MC Alger katika Uwanja wa Orlando jijini Johannesburg huko Afrika Kusini.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Algiers, Algeria, Orlando Pirates iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika hatua ya nusu fainali, Mamelodi Sundowns itakutana na Al Ahly na Pyramids FC itaumana na timu itakayosonga mbele baina ya Orlando Pirates na MC Alger.
Mechi za kwanza za hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitachezwa kati ya Aprili 18 na 19 mwaka huu na michezo ya marudiano itachezwa kati ya Aprili 25 na 26.