Aliyeua ndugu watatu, ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Arusha.”Ni mauaji ya kusikitisha.” Ndivyo unavyoweza kusema baada ndugu watatu ambao Ester Matei, Lidia Matei na Anjela Barnaba kuuawa kwa kuchomwa visu sehemu mbalimbali za miili yao.

Mauaji hayo yalitokea Septemba 18, 2022 katika Kijiji cha Mchangani ambapo Anjela (marehemu) alikwenda kufanya usafi kwenye kaburi la baba yake akiongozana na watoto wa ndugu zake Ester na Lidia (marehemu).

Walipofika katika eneo hilo hawakukuta msalaba katika kaburi hivyo kulazimika kuanza kutafuta maeneo ya jirani,  wakiwa wanaendelea alitokea kijana mmoja aitwaye Matei ambaye alikuwa mjukuu wa marehemu mwenye shamba, aliyewaamuru kuondoka.

Ilidaiwa Ester alimjibu kuwa wanatafuta msalaba wa babu yao, ambapo Matei alidaiwa kumpiga na ubapa wa panga na kuwataka waondoke, Matei alielezwa kuondoka na baada ya muda mfupi kurejea akiwa na mshtakiwa (Raymond Milanzi) ambaye alimchoma Ester kifuani, Anjela juu ya kwapa la kulia ambapo baadaye wote watatu (Ester Matei, Lidia Matei na Anjela Barnaba) walifariki dunia shambani humo.

Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mtwara, imemhukumu Raymond Milanzi, adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kumkuta na hatia ya mauaji ya watu hao watatu.

Jaji Martha Mpaze, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji, alitoa hukumu huyo Aprili 4, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama ambapo baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili amesema upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka.

Ilivyokuwa

Shahidi wa nne wa mashtaka, Hebeti ambaye ni mtoto wa Anjela, alidai wakati wa mashambulizi hayo alikimbilia kijijini kwa ajili ya kuomba msaada na waliporudi eneo la tukio walikuta watu wote watatu wamefariki dunia.

Katika hukumu hiyo Jaji Mpaze amesema licha ya kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja, mazingira ya mauaji hayo yameonyesha uwezekano wa kuwepo kwa mgogoro wa ardhi baina ya mshtakiwa na marehemu hao.

Shahidi wa nne alidai siku ya tukio mama yake alimchukua hadi Mchangani kwa ajili ya kusafisha kaburi la babu yake, Hebeti Mshungeni, na wakiwa njiani walikutana na binamu zake (Lidia na Ester) na kuongozana nao hadi kwenye shamba lililokuwepo kaburi hilo.

Alidai walipofika waligundua kuwa msalaba haukuwepo, hivyo kuanza kuutafuta maeneo ya jirani katika shamba hilo.

Wakati shahidi huyo akiwa ndiye shahidi pekee wa tukio hilo, mashahidi wengine walichukua jukumu muhimu katika kesi hiyo, wakitoa maelezo ya ushiriki wao na hatua walizochukua kufuatia uhalifu.

Shahidi wa kwanza, Dk Rajab Nasoro, aliyeufanyia uchunguzi miili hiyo mitatu alihitimisha kuwa wote walipoteza maisha kwa kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha makubwa ya kuchomwa na visu.

Shahidi huyo alitaja jeraha la Ester lililokuwa kifuani lilikuwa na urefu wa sentimita saba, jeraha la Lidia upana wa sentimita nne na urefu wa sentimita sita na la Anjela lilikuwa na urefu wa sentimita sita na upana wa sentimita nne.

Shahidi wa tatu, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Machinda, Anjelina Joseph alidai kupokea taarifa za mauaji hayo kutoka kwa mpita njia ya kuzifikisha kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji.

Alidai baada ya tukio hilo, usiku aliongozana na Maofisa Polisi kwa ajili ya upekuzi katika nyumba ya mshtakiwa, ambapo walipata kisu kinachoshukiwa kuwa silaha iliyotumika kwenye mauaji hayo.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, hata hivyo, kwa sababu zinazojulikana na upande wa mashtaka, kisu hicho hakikuwahi kutolewa kama kielelezo mahakamani.

Shahidi wa tano, Sajenti Boaz ambaye alikuwa mpelelezi katika kesi hiyo alidai Raymond alijisalimisha siku hiyo ya tukio, kwa hiari katika Kituo cha Polisi cha Nachingwea na kukiri kuhusika na mauaji hayo na baada ya kumjulisha haki zake za kisheria, aliandika maelezo yake.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Raymond alikana kutenda kosa hilo na kudai kesi hiyo ni ya kutungwa kutokana na na mgogoro wa ardhi unaoendelea.

Alidai kuwa siku hiyo ya tukio alikutana na kundi la watu saba wakiwamo marehemu hao, shahidi wa nne, Valency Matei, Charles Matei na mtu mmoja aliyekuwa akiongozana nao ambaye alikuwa akitaka kununua eneo hilo lenye mgogoro.

Alidai kuwa baada ya kuhoji uwepo wao, ugomvi ulitokea na kundi hilo lilikuwa na silaha na kumshambulia ambapo alipata majeraha na kuwa marehemu hao walijeruhiwa wakati wa ugomvi huo.

Raymond alikana kuhusika na mauaji hayo wala kuhusika na shambulio lolote, akisisitiza kuwa anahusishwa isivyo haki kutokana na mzozo wa ardhi.

Uamuzi Jaji

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili Jaji Mpaze amesema katika kesi za jinai upande wa mashtaka unabeba jukumu la kuthibitisha hatia ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote.

Jaji Mpaze amesema kifungu cha 3(2) (a) cha Sheria ya Ushahidi, kimefafanua kuwa mambo muhimu yanayopaswa kuthibitishwa katika kosa la mauaji ni pamoja na endapo kifo kilichotokea hakikuwa cha asili, mtuhumiwa ndiye alisababisha kifo hicho pamoja na mtuhumiwa alitenda kosa hilo kwa nia mbaya.

Amesema hakuna ubishi kuwa vifo vya Anjela, Lidia na Ester walifariki baada ya kutokwa na damu na nyingi na ni jambo lisilopingika kuwa vifo hivyo havikuwa vya kawaida kwani vilitokana na majeraha mabaya ya kuchomwa kisu.

Kuhusu uhusika wa mshtakiwa katika mauaji hayo alidai shahidi wa nne ndiye shahidi pakee wa kuaminika ambaye alieleza jinsi Raymond alivyotekeleza shambulio hilo, huku mshtakiwa huyo akikiri kuwa hana mgogoro wa aina yoyote na shahidi wanne na hivyo inaondoa uwezekano wa uzushi kwa mshtakiwa huyo.

Jaji amesema Raymond hakumhoji shahidi wa nne kuhusu idadi ya waliokuwepo shambani wala shahidi wa tano aliyedai kuwa alijisalimisha polisi mwenyewe na kuwa kwa kushindwa kuhoji hayo kunadhoofisha uaminifu wake.

Kuhusu kisu kilichotajwa na shahidi wa tatu kuwa kiliokotwa nyumbani kwa mshtakiwa, lakini hakikutolewa kama kielelezo mahakamani, Jaji amesema kinaacha mapengo katika kesi ya mashtaka na kuwa kingetolewa kingeonyesha uhusiano wa ushahidi kuhusu mshtakiwa na kosa hilo.

Jaji Mpaze amesema kukosekana kwa kisu pekee hakuondoi hatia kwa mshtakiwa huyo kwani ushahidi wa kimazingira pia unaunga mkono kesi ya upande wa mashtaka.

“Kutokana na ushahidi huo sina shaka kuwa ni Raymond ndiye amehusika na vifo vya Ester, Lidia na Anjela. Utetezi wake, kwamba huenda alihusishwa na kesi hii kutokana na mgogoro wa ardhi unaoendelea, hauna mashiko,”amesema Jaji.

Kuhusu mtuhumiwa kutenda kosa hilo kwa nia mbaya, Jaji Mpaze amesema waathirika wa tukio hilo walipata majeraha makubwa, yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali kama kisu, hivyo mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa nia mbaya.

“Zaidi ya hayo, waathirika walikuwa wanawake wazee, walioainishwa kama watu wasio na uwezo chini ya sheria, kulingana na ripoti ya uchunguzi wa maiti, walikuwa na umri wa miaka 76, 68 na 58. Kwa kuzingatia umri wao na udhaifu wao wa kimwili, hawakupata nafasi yoyote ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya vurugu,” amesema Jaji.

Jaji Mpaze alihitimisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi yake bila shaka yoyote na kuwa Mahakama inamtia hatiani Raymond na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *