Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini, vyama vya siasa na mashirika yasiyo ya kiserikali, kuhamasisha wananchi wazingatie amani na utulivu wakati wa uchaguzi.
Ametaka hilo liambatane na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kuwachagua viongozi.
Majaliwa anakuja na kauli hiyo katika kipindi ambacho, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinahamasisha wanachama wake kuzuia uchaguzi kupitia ajenda yake ya hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi ‘No Reforms No Election.’
Ajenda hiyo kwa mujibu wa Chadema, inalenga kuushinikiza umma kuandamana siku ya uchaguzi ili kuuzuia, kushinikiza mageuzi ya sheria na kanuni zinazohusu uchaguzi.
Majaliwa ameyasema hayo leo, Jumatano, Aprili 9, 2025 katika hotuba yake kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/26.

“Niwasihi viongozi wa dini, vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya serikali na viongozi wote kuendelea kuhamasisha wananchi wote kuzingatia amani na utulivu wakati wa uchaguzi, lakini pia kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kuwachagua viongozi,” amesema.
Majaliwa amesema INEC imeendelea kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu, kwa kuratibu na kusimamia uboreshaji wa daftari hilo.
Hadi Machi 2025, amesema uboreshaji awamu ya kwanza umekamilika katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar na maandalizi ya awamu ya pili yanaendelea.
“Nitumie nafasi hii kutoa rai kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza kuhakiki taarifa zao kwenye daftari kabla kuhitimishwa kwa awamu ya pili ya uboreshaji,” amesema.
Ameambatanisha hoja hiyo na ufafanuzi kuhusu hali ya siasa na utekelezaji wa demokrasia nchini, akisema imeendelea kuimarika kutokana na maboresho ya mifumo na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali.
“Moja ya jitihada hizo ni marekebisho ya sheria ili kuimarisha utawala wa demokrasia nchini. Bunge lilitunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024; Sheria ya 68 Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 2 ya Mwaka 2024 na kufanya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258. Serikali kwa upande wake tayari imeshakamilisha utungaji wa Kanuni za Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,” amesema Majaliwa.