Kipengele cha kuzuia ‘kusevu’ picha, video WhatsApp mbioni kuletwa

Dar es Salaam. Huenda ikawa habari njema kwa watumiaji wa mtandao wa WhatsApp katika kutunza siri na faragha zao kutokana na hatua mpya ya kuzuia kuhifadhi picha video na mazungumzo, iliyopo mbioni kuletwa.

Mtandao huo unaomilikiwa na kampuni ya Meta huenda ukaruhusu kuzuia watu kuhifadhi picha na video pamoja na kuchukua kusafirisha mazungumzo yenu ‘Chart Exporting’. Kwa mujibu wa The Indian Express.

Hatua hiyo imetajwa kuwa habari njema kwani katika kuwasiliana na watu kupitia mtandao huo wapo baadhi ambao huchukua taarifa hizo bila ya muhusika kujua.

Kipengele hicho cha faragha kwa mujibu wa ripoti ya WABetaInfo, kitafanya kazi kwa njia inayofanana na Disappearing Messages (ujumbe unaotoweka), ambapo mtu ataweza kuona picha au video mara moja tu bila kuwa na uwezo wa kuipakua au kuihifadhi kwenye simu yake.

Kwa sasa, WhatsApp inaruhusu mtu kusafirisha historia ya mazungumzo, lakini kipengele hiki kipya kitaondoa uwezo huo kwa watumiaji ambao wamekiwasha.

Hata hivyo, kipengele hiki bado kipo kwenye hatua za mwanzo za maendeleo ingawa kitakuwa cha hiari mtumiaji ataweza kukiwasha au kukizima.

Lengo lake kuu ni kulinda taarifa nyeti na binafsi dhidi ya kuhifadhiwa au kuchukuliwa bila ruhusa.

Faida zake zimetajwa kulinda picha na video binafsi zisihifadhiwe na mtu mwingine. Kuzuia kusambazwa kwa historia ya mazungumzo bila idhini sambamba na kutoa usalama zaidi kwenye mazungumzo ya siri au nyeti.

Inakadiriwa kipengele hiki kinaweza kuchukua wiki au miezi kadhaa hadi pale kitakapoanza kutumiwa rasmi kwa watumiaji wote duniani.

Aidha tovuti ya beebom imesema kipengele hicho kinachoitwa ‘Advanced Chat Privacy’  kitaboresha usalama wa watumiaji, kitawajulisha kama kipengele hiki kimewashwa au kimezimwa, kuongeza uwazi kwenye mazungumzo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka WABetaInfo, toleo jipya la beta (2.25.11.2) kwa watumiaji wa Android inaonyesha kipengele hiki kitazuia huku kikitoa ujumbe wa onyo kuwa haitawezekana unachotaka kufanya.

Vilevile kitatoa taarifa kwa wote kwenye mazungumzo pale kipengele hiki kinapowashwa au kuzimwa iwe kwenye chat binafsi au kwenye grupu.

Hata hivyo bado haijathibitishwa kama kipengele kitaweza pia kuzuia watu kupiga screenshot. Hilo linasubiriwa kufafanuliwa zaidi.

Hatua hii inatajwa kuwa ni moja ya maboresho makubwa ya faragha kwenye WhatsApp, hasa kwa wale wanaotuma taarifa nyeti au binafsi. Kuna pendekezo kwamba WhatsApp ingeweza kuzuia pia forward ya ujumbe bila ruhusa na screenshot ya chat yenyewe.

Mtumiaji wa WhatsApp, Anna Michael kutoka Dar es Salaam anasema ni habari njema kwani itazuia watu kuingiliana faragha na taarifa nyeti zao.

“Sasa hivi watu hatuaminiani tunachati kwa mashaka hatua hii ni bora kwa upande wangu imenifurahisha,” amesema Anna.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *