
Dar es Salaam. Watumiaji wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) wanaotumia akaunti bandia zenye majina ya watu maarufu, maarufu ‘parody accounts’, kuanzia Aprili 10, 2025 watalazimika kujitambulisha wazi ili kuepuka kuchukuliwa hatua kali.
Hatua hiyo imechukuliwa na kampuni ya X inayomilikiwa na tajiri wa dunia, Elon Musk, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha sheria dhidi ya matumizi ya akaunti bandia au zile zinazojifanya kuwa watu wengine maarufu.
Kulingana na taarifa ya kampuni hiyo, kuanzia Aprili 10, 2025, akaunti zote zinazojifanya au kuiga mtu mwingine zitapaswa kutumia maneno kama “bandia” au “utani” mwanzoni mwa jina la akaunti, ili kuonyesha wazi kuwa si rasmi.
Aidha, watumiaji wa aina hiyo watalazimika kutumia picha tofauti kabisa na zile zinazotumiwa na akaunti halisi wanazojaribu kuiga.
Kwa muda mrefu, watumiaji wa X wamekuwa wakilalamikia mkanganyiko unaosababishwa na akaunti za bandia, hasa zile zinazojifanya kuwa watu maarufu kama Elon Musk mwenyewe.
Kupitia taarifa yake iliyonukuliwa na BBC, kampuni ya X ilisema: “Mabadiliko haya yanalenga kusaidia watumiaji kutambua kwa urahisi kuwa akaunti hizo si rasmi, na kupunguza hatari ya udanganyifu au kujifanya mtu mwingine.”
Wamiliki wa akaunti hizo wametakiwa kubadili maelezo ya akaunti zao kabla ya utekelezaji wa sheria hiyo mpya.
Sheria hizo zitawahusu pia wamiliki wa akaunti za mashabiki au wale wanaochapisha maoni kuhusu watu maarufu, mfano “CR7 Fans” na nyinginezo zinazohusiana na watu mashuhuri.
Baadhi ya watumiaji wa X wamesema hatua hiyo itaondoa mkanganyiko kutoka kwa akaunti bandia.
Kwa sasa, zipo akaunti nyingi za utani zinazojifanya kuwa Elon Musk au watu wengine mashuhuri zenye mamilioni ya wafuasi na kuchapisha maudhui ya vichekesho, memes, hadi matangazo ya zawadi kama magari na sarafu za kidijitali.
Mfano, moja ya akaunti maarufu ya utani ya Elon Musk yenye zaidi ya wafuasi milioni moja iliandika chapisho likieleza: “Like na comment ili upate nafasi ya kushinda gari la Tesla.” Ujumbe huo ulipata zaidi ya ‘likes’ 428,000 na maoni zaidi ya 200,000.
Kabla ya hatua hiyo, X iliwahi kuweka alama maalumu za utambulisho kwa akaunti za utani kama njia ya kusaidia kuzitofautisha na akaunti halisi, ikiwa ni jitihada za kuimarisha usalama na kupunguza udanganyifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Koncept Group, Krantz Mwantepele, amesema kuwa hatua hiyo ina manufaa na changamoto.
“Ni hatua nzuri kwa sababu inaleta uwazi zaidi na inaweza kusaidia kupunguza upotoshaji wa habari. Lakini kwa upande mwingine, itazuia ubunifu na ucheshi, hasa kwa wale wanaotumia ucheshi kuikosoa jamii. Kuna hofu kuwa uhuru wa kusema na ubunifu wao unaweza kufifia,” amesema.
Mtumiaji wa X, David David, amesema kuwa akaunti bandia zimekuwa zikitumika kueneza taarifa zisizo sahihi au zenye nia ovu dhidi ya watu maarufu au viongozi wa Serikali.
“Hatua hii ni nzuri kwa kuwa itaondosha sintofahamu na mkanganyiko. Kilichobaki ni utekelezaji tu,” amesema David.
Hussein Msinika, maarufu Mcinika wa Lamar, amesema sheria hiyo inalenga kulinda watumiaji dhidi ya udanganyifu na mkanganyiko.
“Kwa muda mrefu akaunti za parody zimekuwa zikichanganya watu, wakidhani wanawasiliana na watu halisi, hasa wale wanaoigiza viongozi au watu maarufu,” amesema.
Akitaja faida, amesema sheria hiyo itasaidia kutofautisha kwa haraka kati ya akaunti halisi na za utani, kulinda watumiaji dhidi ya utapeli na taarifa potofu, na kuhakikisha uwazi pamoja na uwajibikaji wa maudhui yanayochapishwa.