Angola. Tanzania na Angola wametiliana saini mikataba miwili yenye lengo la kuimarisha uhusiano baina ya nchi mbili hizo.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na wa rasimu ya mkataba wa ushirikiano katika sekta ya ulinzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Luanda nchini Angola, leo Jumanne Aprili 8, 2025, Waziri wa Ulinzi na Jeshin la Kujenga Taifa wa Tanzania, Dk Stagomena Tax amesema mkataba huo unalenga kuimarisha ulinzi na usalama wa pande zote mbili.

“Pia, unalenga kushirikiana katika sekta ya afya; michezo, utamaduni na jamii na katika maeneo mengine yenye masilahi kwa pande zote mbili,” amesema waziri huyo.
Waziri Tax amesema mkataba huo utadumu kwa miaka mitano na baada ya kuisha muda wake, pande zote zitaanza mazungumzo mengine kwa ajili ya kuhuisha mkataba huo pamoja na kuongeza maeneo mengine ya kushirikiana ikiwa yatajitokeza.
Tanzania pia imesaini Rasimu ya Hati ya Makubaliano (MOU) Kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wakala wa Uwekezaji Binafsi Ukuzaji na Uwezesha Usafirisha Nje Angola (Apex)
Hati hiyo ya makubaliano inalenga kukuza uwekezaji wa ndani na wa kigeni nchini Tanzania na Angola.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Luanda nchini Angola leo Aprili 8, 2025.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri amesema mkataba huo unalenga pia kuanzisha ushirikiano wa kimkakati baina ya Tanzania na Angola kwa lengo la kuwezesha na kukuza uwekezaji wenye masilahi ya kiuchumi kwa nchi zote mbili.
“Tunalenga kuzingatia miongozo na kanuni za usawa, ushiriki wa hiari, uaminifu na manufaa ya pamoja kama kuanzisha ushirikiano wa pamoja na kwa faida kati ya taasisi hizi mbili,” amesema Teri.
Amesema lengo lingine ni kukuza ushirikiano wa kidiplomasia kwa lengo la kuendelea kuvutia uwekezaji na wawekezaji sambamba na kukuza biashara ya mauzo ya nje na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kiteknolojia.
Rais wa Tanzania, Samia suluhu Hassan yuko Angola kwa ziara ya kikazi ya siku tatu iliyoanza jana Jumatatu, Aprili 7, 2025 na itahitimishwa kesho Jumatano, Aprili 9.
Katika siku ya pili ya ziara ya Rais Samia, leo asubuhi, ameweka shada la maua katika kaburi la muasisi wa Taifa la Angola, Antonio Agustino Neto na ameshuhudia utiliwaji wa saini wa hati hizo za makubaliano akiwa na mwenyeji wake Rais João Manuel Loureiro.