
Dodoma. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema tangu ateuliwe kuongoza wizara hiyo haridhishwi na maendeleo yaliyopo kwenye zao la chai kutokana na mambo yanayoendelea ikiwamo kushuka kwa mapato yatokanayo na mauzo yake nje ya nchi.
Bashe ameeleza hayo leo Aprili 8, 2025 wakati akizindua bodi mpya ya wakurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania (TBT) kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa tasnia ya chai nchini uliofanyika jijini hapa akisema wasafirishaji hawaelewi kwa uwazi kiasi wanachokipeleka nje ya nchi na kiasi kinachozalishwa nchini kinashuka kila mwaka.
Katika mkakati wa kuongeza mchango wa sekta ya chai nchini, Bashe amemuagiza mwenyekiti wa TBT ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB pia, Abdulmajid Nsekela kuhakikisha anatumia uzoefu wake katika sekta ya fedha pamoja na uzoefu walionao wajumbe wake kushughulikia changamoto zinazorudisha nyuma maendeleo ya chai nchini.
“Tulipokuwa tunatafuta mwenyekiti mpya wa Bodi ya Chai Tanzania tulisema tumpate mtu anayetoka sekta ya fedha atakayeijua sekta ya chai ambayo changamoto yake kubwa ni upatikanaji wa mikopo ili ashiriki kuitatua changamoto hiyo na kuifanya sekta hii ikue na kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye kipato cha wakulima na wadau wa sekta ya chai pamoja na kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa,” amesema Bashe.
Baada ya kumpata mwenyekiti, amesema waliwatafuta wajumbe wenye ujuzi na uzoefu katika sekta tofauti ikiwamo masoko ili wasaidie kuweka mkakati wa kuitengenezea nembo imara chai ya Tanzania itakayoiwezesha kushindana kimataifa.
Kwenye maelekezo yake kwa bodi hiyo ya wakurugenzi pamoja na menejimenti ya TBT, Waziri Bashe amesema changamoto zote zilizopo kwenye sekta ya chai ni mfumo wake, hivyo ameitaka bodi ya wakurugenzi kupitia mpango mkakati wa TBT pamoja na sera ya chai na kutoa mapendekezo, yatakayosaidia kuziondoa kero zilizopo.
“Hakikisheni kunakuwa na uwazi wa taarifa kwa sababu baadhi ya wasafirishaji ambao hawaisajili mikataba yao yote, hivyo kuinyima Serikali taarifa sahihi. Kwa msafirishaji atakayebainika kutotoa taarifa za mzigo anaosafirisha afutiwe leseni. Sekta ya chai inao wadau wasiopenda kukutana, kila mmoja anataka afanye mambo yake kivyake. Undeni kamati itakayowahusisha wadau wengine kuangalia namna ya kuyashughulikia matatizo tuliyonayo ili tuwe na chai bora zaidi,” amesisitiza Waziri Bashe.
Akionesha utayari wa kuyatekeleza maelekezo hayo, Nsekela aliyeteuliwa Februari 2025 kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TBT amesema anayo imani watazishughulikia kero zilizopo na kuifanya sekta ya chai kuwa na mchango mkubwa zaidi kuanzia kwa wakulima mpaka viwanda vinavyolichakata zao hilo.
“Tunahitajia maridhiano kwa kuwajumuisha wadau wote katika sekta ya chai. Asiwepo anayefaidi zaidi ya mwenzake. Ni lazima tufanye mabadiliko ya uwazi. Kila mdau awe na atoe taarifa sahihi. Katika hatua hizo zote, tutahitaji ustahimilivu wa kuleta maboresho tunayoyakusudia. Tutafanya marekebisho muhimu katika mnyororo mzima wa zao la chai na tukisikilizana, tutafanikiwa kujenga pamoja,” amesema Nsekela.
Licha ya uzoefu wake mkubwa katika sekta ya fedha nchini, Nsekela pia anaifahamu sekta ya kilimo, alikuwa mwenyekiti wa Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHTDA) kabla haujaunganishwa na TBT hivi karibuni na ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania.
Tanzania kuna wakulima wadogo 32,000 wa chai huku wananchi wengine zaidi ya milioni mbili wakipata ajira zisizo za moja kwa moja katika sekta hiyo. Kuanzia Desemba 2024 hadi Machi 2025, Tanzania imeingiza Sh50.25 bilioni kutokana na vibali vya kusafirisha chai nje ya nchi vinavyotolewa na TBT.
Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imewavutia wawekezaji waliowekeza katika maeneo ya Kilolo, Njombe na Mbeya. Aidha, wawekezaji na wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali duniani wameendelea kujitokeza ili kuwekeza na kununua chai ya Tanzania.
Akizungumzia baadhi ya kero zilizopo, mwenyekiti wa wakuu wa wilaya kutoka halmashauri zinazolima chai nchini, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffer Haniu ameitaja bei ndogo ya majani mabichi ya chai na kuchelewa kwa malipo ya wakulima pamoja na kufungwa kwa viwanda vya chai kuwa kunawakatisha tamaa wakulima.