Kuna nini Dar City BDL?

WAKATI timu zikiwa katika maandalizi kwa ajili Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) msimu ujao,  Dar City inaweza kushindwa kuonyesha makali kunatokana na kutoaanza mapema mazoezi ya pamoja.

Timu hiyo yenye wachezaji wazoefu kutoka ndani na nje ya nchi, inadaiwa kuonyesha kujiamini zaidi kabla ya kuanza kwa msimu.

Wachezaji nyota wa Dar City ni pamoja na Mmarekani Jamel Marbuary, Wakenya Victor Mwoka na Bramwel Mwombe pamoja na wazawa Erick John, Ally Abdallah na Haji Mbegu.

Hata hivyo, kujiamini kunaweza kuifanya isifanye vizuri katika ligi hiyo kutokana na ubora wa timu na maandalizi yanayofanywa na timu zingine.

Akizungumzia maandalizi ya timu za kikapu kuelekea msimu ujao, mmoja wa mashabiki na wadau wa mchezo huo jijini humo, Athuman Maulid ameliambia Mwanaspoti kuwa amekuwa akifuatilia mazoezi ya tumu mbalimbali, lakini Dar City haijaanza.

“Inawezekana kama inavyodaiwa kwamba wamefanya usajili mzuri, lakini hiyo haina maana sana hata kama una wachezaji wengi wakubwa na bora,” alisema Maulid.

Kocha wa timu hiyo, Mohamed Mbwana alikiri kuwa hawajaanza mazoezi ya pamoja ya maandalizi ya ligihiyo, lakini wachezaji wamekuwa wakifanya katika maeneo tofauti.

“Nimekuwa nikiwafutilia, wako vizuri, siyo muda mrefu tutawaita kwa ajili ya kuanza mazoezi ya pamoja,” alisema Mbwana.

Kamishna wa Ufundi na Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), Haleluya Kavalambi alisema mashindano hayo yataanza mwezi huu, ambapo tarehe itatangazwa baada ya kikao cha uongozi wa Chama cha Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD) na klabu shiriki ili kupitia kanuni na kuzipitisha. 

Timu za wanaume zitakazoshiriki ligi hiyo ni JKT, UDSM Outsiders, Dar City, ABC, Chui, Pazi, Polisi, DB Oratory, KIUT, Mgulani JKT, Srelio, Stein Warriors, Kurasini Heat, Vijana ‘City Bulls’, Mchenga Star na Savio.

DAR
DAR

KURASINI YATOA VITISHO

NAHODHA wa Kurasini Heat, Dominic Zacharia ametamba kuwa wamejipanga kuzinyoosha timu watakazokutana nazo katika ligi hiyo.

Kurasini Heat ilianzishwa mwaka 2009 na 2020 ilikuwa bingwa wa BDL baada ya kuifunga JKT kwa michezo 3-1.

Jeuri ya nahodha wa timu hiyo imekuja baada ya wachezaji wenzake kuahidi kufanya makubwa wakilenga kubeba ubingwa na kushiriki mashindano makubwa kitaifa na kimataifa.

Akizungumzia maandalizi, Zacharia alisema wanaendelea na mazoezi katika Uwanja wa Bandari uliopo  Kurasini, ambapo wachezaji wote wamekuwa wakihudhuria.

“Tumekuwa tukifanya mazoezi uwanjani kujiweka fiti na baada ya hapo tunaingia kucheza,” alisema.

Kwa mujibu wa nahodha huyo mabosi wao wanakusudia pia kusajili wachezaji wachache wenye uwezo mkubwa  kwa ajili ya kuimarisha kikosi.

“Unajua ligi ya BDL ni kubwa, bila kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa huwezi kufanya vizuri,” alisema Zacharia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *