
Dar es Salaam. Kilele cha shindano la Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu kinatarajiwa kufanyika Aprili 13 mwaka huu, ambapo waandishi 37 watachuana kuwania tuzo hiyo.
Waandishi hao ni katika makundi manne ya kazi za fasihi ambayo ni ushauri, tamthiliya, riwaya na hadithi za watoto katika lugha ya Kiswahili.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tuzo hizo Profesa Penina Mlama, alisema tangu kutangazwa kwa kinyang’anyiro hicho waandishi wameonyesha kuchangamkia kwa kuwasilisha miswada ya kazi zao.
“Kama ilivyokuwa mwaka jana, hamasa imekuwa kubwa zaidi mwaka huu tumepokea miswada mingi orodha kamili itatolewa siku ya tuzo ila iliyoingia kwenye fainali ni miswada 37.
Miswada hii ipo katika makundi manne tamthiliya 10, mashairi 10, riwaya 10 na hadithi za watoto saba. Hadithi za watoto zimekuwa saba kwa sababu hizo ndizo zimekidhi viwango, tusiwengeweza kuweka kazi hata kama hazijakidhi viwango,” alisema Profesa Penina.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni mwandishi mahiri wa fasihi alisema mshindi wa kwanza katika kinyang’anyiro hicho atapata Sh10 milioni na kazi yake itachapwa na kusambazwa shuleni, huku mshindi wa pili akipata Sh7 milioni, mshindi wa tatu Sh5 milioni na mshindi wa nne hadi wa 10 wakipata vyeti.
Kwanini tuzo hii
Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali ilidhamiria kutoa tuzo hiyo na kuipa jina la Mwalimu Nyerere, kwa ajili ya kumuenzi kiongozi hiyo aliyekuwa na mapenzi makubwa na uandishi wa fasihi.
“Shughuli itafanyika siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Mwalimu Julius Nyerere ambaye si tu muasisi wa Taifa hili, bali ni mwanasiasa maarufu duniani na mwandishi wa vitabu vya fasihi akiandika pia mashairi na kutafsiri kazi za uandishi.
“Kiongozi huyu pamoja na majukumu mazito aliyokuwa nayo katika kuliongoza Taifa na harakati za ukombozi, alitenga muda wake kwa ajili ya kazi za uandishi wa kazi bunifu,” alisema Profesa Mkenda.
Profesa Mkenda alisema pamoja na kumuenzi Mwalimu Nyerere lengo la tuzo hizi ni kuhamisha watanzania wengi wajitokeze kuandika, ili wajue wanapoandika wanaweza kutambuliwa.
Lengo lingine ni kukuza lugha ya Kiswahili na kuhamasisha Watanzania wengi wanaweka maandishi kwenye lugha hiyo adhimu ambayo umaarufu wake unaongezeka siku hadi siku.
Mbali na hilo Profesa Mkenda alisema tuzo hizo zimeanzishwa kwa lengo la kukuza utamaduni wa kujisomea hasa kazi za waandishi wazawa wanaondika kuendana na muktadha wa Kitanzania.
“Mbali na mshindi kupata fedha Serikali itagharamia uchapishaji wa kitabu kuhakikisha kinachapwa na kusomwa katika shule zote. Hii ni heshima kubwa kwa mwandishi.
“Tunataka kuhamasisha usomaji, kuna vitabu vya kiada na ziada ambavyo unaweza kusoma kujiongezea uelewa. Haina maana kupata vitabu sasa viondoe vitabu vya zamani. Huenda baadaye hivi vinavyoshinda vikawa vya kiada.
Lengo lingine kwa mujibu wa waziri huyo ni kuhifadhi historia na maadili ya nchi yetu kupitia maandishi ya fasihi yanayoandikwa na waandishi wazawa.
Alisema hakuna nchi inayoweza kutambulika bila utamaduni, hivyo kuweka msisitizo kwenye uandishi bunifu ili maandiko yabebe taswira ya utamaduni wa Mtanzania.
“Ni wajibu wetu kukuza uandishi ambao unachambua mazingira yetu kama ambavyo tunasoma vitabu vya wenzetu wanaoeleza mambo yao na tamaduni zao ambazo na sisi tunaziiga.
“Changamoto kubwa ya dunia sasa ni aina ya maandishi yanayokuza baadhi ya maadili yanayokinzana na maadili yetu.
Hivyo ni muhimu kuwa na watu wanaoandika vitabu kuhusu maadili yetu kuliko kupoteza muda mwingi kuzuia vile vinavyoharibu maadili,” alisema.