
Dar es Salaam. Kuwekeza katika kilimo cha kisasa na viwanda ni miongoni mwa maeneo matano yaliyoainishwa na wadau, kama muhimu kwa Serikali katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Pia, wadau wanasema kwamba utekelezaji wa maeneo hayo unaweza kutoa suluhu ya kudumu ya ajira.
Wadau hao wameeleza maeneo hayo leo, Aprili 4, 2025, katika kongamano la kitaifa la ajira, lililowakutanisha wadau mbalimbali kutoka nchini, lilioandaliwa na Chama cha ACT- Wazalendo.
Kongamano hilo limefanyika katika makao makuu ya chama hicho, yaliyopo Magomeni, Jijini Dar es Salaam.
Msingi wa kongamano hilo ulikuwa ni kujadili na kukusanya maoni ya wadau kuhusu njia bora za kushauri Serikali katika kushughulikia suala la ajira, hasa baada ya vijana kuanza kujitokeza hadharani na kushinikiza kupata ajira.
Wakizungumza kwenye kongamano hilo, wamesema kinachotakiwa kufanywa na Serikali ni kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kiwanda cha kuchenjua gesi kuwa kimiminika huko Likong’o, Lindi.
Pia, wamesema Serikali inatakiwa kuanzisha viwanda vya chuma, kupambana na ufisadi na kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha mishahara inaendana na gharama za maisha.
Wadau hao waliainisha maeneo hayo, leo Aprili4,2025 kwenye kongamano la kitaifa wa ajira uliowakutanisha wadau mbalimbali nchini ukiandaliwa na Chama cha ACT Wazalendo, uliofanyika makao makuu ya chama hicho Magomeni Jijini Dar es Salaam.
Msingi wa kongamano hilo ni kujaribu kukusanya maoni na kupata mawazo mapya namna gani wanaweza kupata njia na kuishauri Serikali kuona cha kufanya baada ya vijana kuanza kujitokeza hadharani kuishinikiza serikali kuwaajiri.
Akianza kuchokoza mada katika kufungua kongamano hilo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema Tanzania tatizo la ajira linazidi kuwa kubwa na linawakumba vijana kwa asilimia 70 waliopo chini ya miaka 35.
“Tanzania asilimia 55 ni nguvu kazi katika makundi mengine, lakini nchi yetu ukitamka changamoto ya ajira unaonekana mchochezi viongozi wanashindwa kuchukua hatua kukabiliana na uhaba wa ajira na badala yake wanajitetea kwa kusema tatizo la ajira si la Tanzania pekee bali ni dunia nzima,” amesema.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo- Bara, Isihaka Mchinjita amesema Serikali kupuuza maendeleo ya sekta zinazoweza kuzalisha ajira kwa wingi kama vile viwanda, gesi, kilimo na teknolojia ni sababu ya kuongezeka kwa tatizo la ajira.
“Mfano sekta ya kilimo, ambayo inaajiri asilimia 60 ya Watanzania ina mchango wa asilimia 26 kwenye pato la Taifa. Hata hivyo, ukuaji wake ni chini ya asilimia tano, wakati bajeti ya Serikali kwa sekta hii, ambayo ina mchango mkubwa katika mapato ya Taifa na inaathiri maisha ya wananchi wengi ni chini ya asilimia tatu,” amesema.
Mchinjita amesema kiwanda cha kuchenjua gesi kuwa kimiminika huko mkoani Lindi, kitakapokamilika, kinaweza kuzalisha ajira 10,000.
Hata hivyo, mnyororo wake wa thamani ungeweza kutoa ajira nyingi zaidi, hasa ikiwa viwanda vya saruji na plastiki vitajengwa baada ya kuendelezwa mradi huo.
“Kuna mradi kama huo unafanyika Msumbiji eneo la Palma, na kampuni zinazofanya huko zilianza kufanya uchunguzi kwetu tukayawekea kauzibe, lakini wenzetu yanafanya kazi,” amesema.
Kulingana na Mchinjita amesema Tanzania licha ya kuwa na makaa mengi ya mawe, lakini inatumia fedha nyingi kuagiza chuma kutoka nje ya nchi kila mwaka fedha ambazo zingeweza kutumika kuzalisha chuma nchini.
“Tuna makaa ya mawe mengi, nchi nyingi zinajenga reli tungekuwa tunawauzia na fedha hizo zingeingia nchini na tungekuwa na za kuzalisha ajira nyingi lakini miradi hiyo imebaki kwenye makaratasi,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa ACT Wazalendo, Riziki Mungwali amesema vijana wanatakiwa kupewa ujuzi maalumu, maarifa na elimu ya vitendo isiwe ile ya kuifanyia mitihani bila kuifanyia kazi.
“Iwe elimu inayomwezesha mtu kujifunza katika maeneo mengine hata ukiangalia falsafa ya nchi yetu katika elimu ni vitu viwili tofauti na kinachoendelea kwenye jamii yetu, hatujengi elimu ya kujitegemea kwa kuwafanya vijana kuwa na udadisi wa kutosha ili waweze kujifunza.
Kiongozi kutoka Umoja wa Vijana Wasio na Ajira Tanzania (UYAM), Laurent Akido amesema kuwa nchini Tanzania, vijana wengi wametengwa na maamuzi yao ambapo watu wazima ndio wanaamua kwa niaba yao.
Amesema hii ni tofauti na mataifa mengine yaliyoendelea, ambapo vijana wanakuwa na nguvu ya kushika hatamu katika nafasi kubwa za kiserikali.
“Hapa Tanzania, kijana wa miaka 35 bado anakaa kwa wazazi, na hili lina hatari kubwa. Ndiyo maana tunasema hatutatulia hadi soko la ajira litulie na Serikali ihakikishe inatambua kuwa kuna vijana wengi nchini,” amesema.
Amesema pia, licha ya Serikali kutoa wito wa vijana kusomea Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) , ni vigumu kwa vijana wengi kwenda huko kuchukua ujuzi mwingine, kwa sababu wanataka kwanza kutumia walionao.
“Leo hii mimi na ukomavu huu angali nikiwa kijana na miaka 35, lakini naonekana mtu mzima kama nina miaka 50, unataka unipeleke Veta nikajifunze namna ya kutengeneza au kushona viatu nataka fani niliyosomea iheshimike kwanza,” amesema.
Akiunga mkono msimamo huo, muhitimu wa Chuo cha Usafirishaji, Julius Mussa amesema wito wa kuwahimiza vijana kwenda Veta ni hatua ya kimkakati, na inaonyesha kuwa elimu inayotolewa nchini Tanzania bado haijakamilika, jambo ambalo limekuwa chanzo cha mambo mengi kupindishwa.
Pia, hoja hiyo iliungwa mkono na Linda Simwa, muhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye alieleza kuwa kauli ya Serikali inadhihirisha kuwa mfumo wa elimu na ajira uliopo hauleti matokeo chanya, na badala yake imekuwa sababu ya vijana kuelekezwa katika elimu ya Veta.
“Ni swali la kujiuliza: Je, wale wote waliomaliza Veta wana ajira? Ukiangalia ajira za Veta, kwa wale waliohitimu na kujiajiri, nyingi ni za muda mfupi na anategemea mteja aje. Ikiwa mteja hatakuja, atajiendesha vipi kimaisha?” amesema na kuhoji.