AKILI ZA KIJIWENI: Hizi ni habari njema kabisa kwa Fei Toto

KILA dirisha la usajili, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ni lazima azue mjadala hapa kijiweni maana haliwezi kupita bila kiungo huyo wa mpira kuhusishwa na mambo ya usajili iwe kwa klabu za hapa ndani au za nje.

Ilianzia tangu alipokuwa Yanga na hata baada ya kujiunga na Azam FC jambo ambalo haliji kwa bahati mbaya bali ni kutokana na uwezo wake mkubwa anaouonyesha ndani ya uwanja katika nafasi ya kiungo.

Na hili la Fei Toto kuwa mchezaji mzuri wala sidhani kama litahitaji kubishana maana mtu yeyote wa mpira anakubaliana nalo labda aibuke mtu ambaye hafahamu bolu aje na vipengele vyake na kupingana na wengi.

Taarifa za usajili kuhusu Fei Toto zimeongezeka zaidi hivi sasa tangu alipojiunga na kuitumikia Azam FC ambapo vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti uwepo wa ofa kemkem za kumuwania ‘Zanzibar Finest’ mwenye umri wa miaka 27 hivi sasa.

Na wakati tunaelekea katika dirisha kubwa la usajili baada ya msimu huu kumalizika tayari kumekuwapo na habari nyingi zinazomhusisha Fei Toto na usajili kwa timu za hapa nyumbani na pia za nje ya Tanzania.

Simba inaripotiwa hailali usingizi kwa ajili ya Fei Toto. Yanga inapigana vikumbo kimyakimya kumrudisha kiungo wao wa zamani. Azam inapambana kumuongezea mkataba na kina Kaizer Chiefs na Wydad Casablanca nao hawako nyuma.

Vyovyote iwavyo, habari hizi ni nzuri zaidi kwa upande wa Fei Toto maana zinamaanisha kuwa atapiga pesa ndefu katika dirisha kubwa la usajili iwe kwa kubakia ndani ya Azam FC au kama akiamua kufungasha virago na kutafuta maisha kwingineko.

Kwa sasa analipwa stahiki nono na Azam FC hivyo akiongeza mkataba ni wazi kwamba maslahi hayo yatazidi na Fei Toto akaunti zake zitanona maradufu zaidi ya ilivyokuwa mwanzo.

Akienda kwenye timu mpya maana yake haitokuwa kwa kiasi cha fedha kidogo au sawa na kila anachokipata Azam FC bali kikubwa zaidi. Kiufupi mkeka wa Fei Toto hauwezi kuchanika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *