Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua kamati kuu mbili zilizopewa jukumu la kuandaa awamu ya pili ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Mkumbi II) ili kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini,
Kuandaliwa kwa mpango huu kunalenga kuangalia changamoto zinazojitokeza katika mazingira ya biashara, kurahisisha kanuni na sheria sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Akizungumza katika uzinduzi uliofanyika leo Aprili 3, 2025 jiji hapa, Majaliwa amezitaka taasisi na mamlaka za udhibiti zitakazohusishwa katika utafiti na tathmini zitoe ushirikiano kwa kamati ili kuja na mapendekezo mahususi yenye malengo mapana yatakayoendana na Dira ya Taifa 2050.
“Hapa ninamaanisha kuwa kamati zitakapokuwa zinafanya tathmini na zinahitaji kupata maelezo, nyaraka kutoka taasisi yoyote ya Serikali, basi taasisi za umma zijue kuwa hii ni kamati rasmi inayofanya kazi rasmi hivyo wapate ushirikiano” amesema.
Majaliwa ameziomba sekta binafsi kutoa mawazo ya kina, mapendekezo yenye manufaa kwa kamati kuhusu maboresho yanayohitajika ili Tanzania iendelee kuwa kivutio cha uwekezaji wa ndani na nje.

“Hivyo ni vyema kuhakikisha jumuiya za wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa zinashirikishwa katika mchakato huu na kupokea maoni ya wadau kuhakikisha maoni yao yanakidhi mahitaji yetu. Wakati hili linafanyika basi taasisi zote zinazohusika na maendeleo ya biashara watoe huduma kwa weledi ili kupunguza urasimu ambao unaweza kusumbua wawekezaji, kuongeza uwazi katika utoaji wa vibali, nyaraka na maeneo mengine,” amesema.
Ameitaka kamati kuhakikisha inaweka vipaumbele kwenye utoaji wa huduma kwa haraka, ufanisi na kukidhi vigezo vya kimataifa ili kuendana na ushindani wa biashara duniani, wawekezaji wanaohamasishwa ni wa pande zote.
Katika hilo, amezitaka mamlaka za udhibiti kuungana katika kufanya kaguzi kwa lengo la kuokoa muda wa wawekezaji wakati mpango wa pili.
Amesisitiza taasisi zinazoweza kufanya kazi pamoja zifanye hivyo ili wawezekezaji na wafanyabiashara watumie muda wao katika uzalishaji.
Amesema wamekuwa wakipata malalamiko hasa eneo la bandarini ambalo lina taasisi nyingi ambazo zinafanya kaguzi za bidhaa.

“Kila taasisi inataka kufanya kazi peke yake kwa utaratibu wake jambo ambalo linachelewesha kutoa mizigo na gharama za uhifadhi wa mzigo bandarini zinaongezeka hii haikubaliki,” amesema.
Amezitaka taasisi zote za kaguzi kuwa na vikao vya pamoja chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambazo kwa pamoja zitafute mfumo utakaorahisisha kukagua bidhaa zinazoingia nchini kwa gharama nafuu na muda mfupi.
Mkurugenzi wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga amesema Mkumbi II ni muhimu hasa kwa dira kuu ambayo itaanza kutekelezwa hivi karibuni ambayo inataka Pato la Taifa la Dola za Marekani trilioni moja na kuongeza kipato cha kila Mtanzania.
“Ili kufanikisha hili ni lazima Mkumbi II iwe kichocheo cha dira hii, itolewe nafasi kwa sekta binafsi kushiriki katika kupanga na kutekeleza maboresho kwani awamu ya kwanza imetufundisha kuwa tunao wajibu katika safari hii ya maboresho,” amesema.
Amesema mpango wa kwanza haukulenga tu mageuzi ya Serikali bali pia ulizitaka jumuiya za kibiashara kuandaa mpango wa kujisimamia zenyewe kama vile kanuni za maadili kwa wanachama wao.
Rais wa Chemba ya Biashara, Kilimo na Viwanda Tanzania (TCCIA), Vincent Minja amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mpango wa kwanza yapo baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kuangaliwa.
Moja ya maeneo hayo amesema ni tozo zinazotozwa na halmashauri ambazo kwa kawaida zinatakiwa kuwa asilimia 0.1 hadi 0.3 lakini halmashauri nyingi zinatoza kiwango cha juu ambacho ni asilimia 0.3.
“Pia kodi hii inatozwa katika mauzo ghafi ukiangalia ni mzigo mkubwa kwenye biashara zetu. Tunapendekeza ifutwe kabisa au itozwe kwenye faida na si mauzo ghafi, inaumiza biashara zetu na kufanya tushindwe kushindana,” amesema.
Waziri Mkuu Majaliwa alizungumzia hilo ameagiza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Mipango na Uwekezaji kuangalia kodi zinatozwa na halmashauri kwa wafanyabiashara ili zisiwe zile zinazowasumbua na kuwaumiza.

“Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kaeni muone na mtupe mwelekeo wa utozaji wa kodi hizi ili zisisumbue wafanyabiashara katika kulipa kodi,” amesema Majaliwa.
Maganga amependekeza kuanzishwa kamati kuu ya maboresho ya udhibiti itakayochambua mapendekezo yote ya kanuni au ada mpya zinazohusu biashara ili kuzuia mizigo mipya isiyo ya lazima.
“Mfano kupitia kamati hii, halmashauri kabla hazijaja na tozo mpya kamati inaweza kupitia kuangalia kuwa tozo hii inayokuja inaendana na mpango wa Mkumbi II, hili litaondoa suala la kila mtu kuanzisha tozo anapohitaji, inakuwa ni changamoto kwenye biashara na hii imekuwa ni sehemu ya kuongeza mapato ya halmashauri,” amesema.