
Mitindo isiyofaa ya maisha ya wazazi na walezi pamoja na kutofuatilia mienendo ya watoto wao, imetajwa kuwa chanzo cha ukatili kwa watoto.
Ripoti ya takwimu za uhalifu na usalama barabarani ya mwaka 2023 iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania, inaonyesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2023 waathirika 15,301 wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, waliripotiwa ikilinganishwa na waathirika 12,163 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
Katika ripoti hiyo, ukatili wenye idadi kubwa ni ubakaji (8,185), ulawiti (2,382), mimba kwa wanafunzi (1,437), kumzorotesha mwanafunzi kimasomo (922) na shambulio la aibu (396).
Ukiondoa idadi hiyo, kwa sehemu kubwa ukatili unatajwa kutendeka ndani ya familia na jamii.
Kidunia, Shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limesema watoto karibu milioni 400 ulimwenguni, wanakabiliwa na ukatili wa kimwili na kisaikolojia nyumbani, kati yao asilimia 60 wapo chini ya miaka mitano.
Takwimu hizo zilizokusanywa mataifa katika mataifa 100 kuanzia mwaka 2010 hadi 2023 zikijumuisha ukatili wa aina zote kwa watoto, zinasema kati ya watoto hao milioni 400, milioni 330 wanapitia ukatili wa kimwili.
Mkazi wa Ngudu Wilaya ya Kwimba, Winfrida John anasema mtindo wa maisha wanaoishi wazazi kuwaacha watoto wajilee wenyewe, unasababisha watoto kukutana na changamoto nyingi ikiwemo kubakwa au kulawitiwa.
Anasema kutokana na mama au baba kutingwa na maisha hata mtoto anashindwa kusema anayopitia kwa vile kwanza hathaminiwi na mzazi, lakini anaogopa vitisho vya mtu anayemtendea ukatili.
Tabia mbaya kwa watoto
Ofisa Ustawi wa jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Leonada Nekidomo anasema mpangilio wa maisha ya wazazi usipokuwa mzuri, unasababisha hata malezi kwa watoto kutokuwa bora kwa kuwa hata viashiria pale watoto wanapofanyiwa ukatili, hawavioni na kusababisha madhara zaidi kutokea.
Anatolea mfano wa tukio la ukatili lililoripotiwa hivi karibuni na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza la mtoto wa miaka 10 kubakwa kwa nyakati tofauti na mwalimu pamoja na mmiliki wa nyumba aliyokuwa anaishi na mzazi wake kuanzia Oktoba, 2024 hadi Februari ,2025.
Anasema mama alikuja kugundua baadaye na hilo linatokana na mpangilio mbaya wa maisha unaofanya wazazi wasiwe na muda na watoto wao.
“Malezi yasipokuwa mazuri kwa watoto kuna athari nyingi sana, mfano watoto kuwa watukutu, kubakwa na kulawitiwa hata kukosa haki ya kupata muda wa kuzungumza na wazazi wao, ‘’ anaeleza na kuongeza:
‘’ Wanashindwa hata kushiriki shughuli mbalimbali za familia yao, kutokana na mzazi kuwa bize na kazi haujui watoto wanaishije wanakula nini kwa hivyo moja kwa moja wataathirika kisaikolojia, kiafya na kijamii pia. Kila mzazi anapaswa kuwajibika katika kusimamia malezi na makuzi ya watoto wao.’’
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilemela, Marwa Mwema anasema kwa asilimia kubwa ukatili unaanzia ngazi ya familia ambao mwishowe baadhi ya wazazi wanatengeneza maridhiano na wanaowatendea ukatili watoto wao.
“Mtoto kwa mfano amefanyiwa tendo la ubakaji lakini cha kushangaza unakuta jamii au familia inakuja kutengeneza maridhiano na yule mkosaji, kwahiyo inaathiri ule utekelezaji wa mchakati mzima wa kukomesha ukatili wa kijinsia,”anasema Marwa.
Anasema ushiriki wa wazazi kwenye malezi ya watoto haupo kwenye msingi mmoja, hivyo malezi yanapolegalega mtoto anachagua mfumo wa maisha huko barabarani.
“Mzazi hajui marafiki wa watoto wake, hajui majukumu gani anafanya baada ya kutoka shule kwahiyo unakuta mtoto anachagua njia mbaya, kwahiyo cha msingi familia ndiyo eneo la kwanza la kutengeneza stadi ya maisha ya mtoto. Wewe mzazi yajue malengo yako, maono, mpe mwongozo, wajue rafiki zake na ujue wanatokea familia gani ili kumtengenezea mtoto ufahamu wa namna atakavyoepuka ukatili,”anasema.
Akisimulia moja ya tukio la ukatili ambalo liliwahi kuletwa ofisini kwake, Marwa anaeleza kuwa viongozi ndio wanaodidimiza na kuyapokea matatizo hayo bila kujali athari za waathirika wa ukatili huo.
“Siku moja mama mmoja alikuja na mtoto akieleza kuwa mume wake alitaka kuuza kiwanja lakini mke wake alimkatalia. Baada ya huyo mama kufuatilia haki yake kwa viongozi hakupata msaada wowote, hatimaye mume aliazimia kuuza nyumba na kiwanja kwa kwa Sh30 milioni. Kwa hiyo mpaka sasa huyu mama amekuwa homeless (hana makazi) na kuhusu watoto hawajui watakula nini na watavaa nini na hata ukiangalia watoto waliopo mtaani watakwambia sababu nyingi zilizosababisha wao kutoka nyumbani ni ukatili,” anasema.
Anaongeza: “Wakati tunatarajia viongozi kwa mfano wa serikali za mitaa kuwa sehemu ya kutatua changamoto hizo na kuwa mabalozi wa kuyaibua, wao ndio wanaohusika katika hayo.’’
Mratibu wa mradi wa Vijana, Elimu, Malezi na Ajira (VEMA) kutoka Shirika la Plan International, Gadiel Kayanda anasema licha ya ukatili kuwa na vyanzo vingi, mara nyingi unatokana na familia kushindwa kulea na kuwajibika ipasavyo kwa watoto wao.
“Suala la malezi katika familia sio la mama peke yake ni la kila mmoja. Kila mtu ana wajibu wa kutoa malezi sahihi. Ikiwa familia haina vyanzo bora vya malezi ni rahisi vijana wengi kufanyiwa ukatili wa kingono au wa kimwili kwa sababu hawana uelewa, hivyo ni muhimu sana kutolewa elimu kuanzia nyumbani hadi shuleni na hata kuchunguza marafiki sahihi wa watoto watakaoendana na malezi ili kuhakikisha ndoto zao zinatimia vyema,”anasema.
Daktari wa magonjwa ya binadamu katika kituo cha Afya Igoma mkoani Mwanza, Dk Violet Sasabo, anasema ipo changamoto ya ya baadhi ya wazazi kushawishiwa kwa pesa ili kufuta ushahidi wa kitabibu au wakati mwingine kuchelewa kumpeleka mwathirika kutibiwa.
“Watoto wengi ambao ni waathirika wa ukatili wanaletwa muda umeshakwenda sana, Kwa mfano ukatili umeshafanyika, imepita wiki au hata mwezi ndipo mzazi anakuja kugundua, anamleta mtoto hospitalini ameshaoshwa hata ukusanyaji wa ushahidi unakuwa mgumu,”anaeleza.
Anasema wakati mwingine kuna baadhi ya wazazi wanaoelewana na wafanya ukatili kisha akifika hospitali anaomba ajaziwe hakuna kilichotokea.
“Nitoe rai kwa jamii, wazazi msikae kimya ingawa wakati mwingine utaona fedheha au aibu. Kutotoa taarifa kwa wakati kunaweza kusababisha athari za kiafya kwa mtoto na kupoteza ushahidi wa mahakama.Ukiwahi kutoa taarifa ya mtoto aliyefanyiwa ukatili anaweza kutibiwa na akaepukana na magonjwa ya kuambukizwa ambayo yanaweza kuzuiliwa kwa wakati,” anasema.
Muuguzi Mkuu Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Agnes Fumbua anasema wazazi kutowafundisha mambo muhimu watoto wao wawapo nyumbani, husababisha kufanyiwa ukatili kirahisi na kuwa vijana wasiokuwa na mwelekeo na maisha.
“Hii leo hakuna mpangilio maalum wa maisha, kwa hivyo, tunashauriwa sisi wazazi au walezi tuwaongoze vijana kuepukana na marafiki wasiofaa na huko ndiko kuna makundi rika au tabia zisizofaa,” anasema.