Moshi kukosa maji kwa saa kadhaa, matengenezo ya bomba yanaendelea

Moshi. Kufuatia hitilafu ya bomba la maji katika Barabara Kuu ya Moshi – Arusha, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Muwsa) imesema baadhi ya maeneo ya Mji wa Moshi yatakosa huduma ya maji kutokana na matengenezo yanayoendelea.

Hitilafu hiyo ya bomba la maji imetokea kwenye eneo la mzunguko wa makutano ya Barabara Kuu ya Arusha – Moshi – Dar es Salaam, hivyo kukatisha huduma ya maji kwa wakazi wa Moshi.

Leo Machi 29, 2025, Mwananchi limefika katika eneo hilo na kushuhudia barabara hiyo ikiwa imefungwa, huku shughuli za uchimbaji wa lami katika eneo ambalo bomba hilo limepita ukiendelea kufanyika.

Jana, Machi 28, 2025, Muwsa kupitia kwa Ofisa Habari wake, Florah Nguma, ilitoa tangazo katika makundi mbalimbali ya WhatsApp ikiwatahadharisha wananchi wa Moshi kuhifadhi maji ya kutosha kufuatia matengenezo ya bomba hilo ambapo maeneo zaidi ya 20 yatakosa huduma hiyo ya maji.

“Naomba kuutaarifu kwamba bomba kuu linalotoa huduma ya usambazaji maji safi limepata hitilafu katikati ya Barabara ya Moshi – Arusha na hivyo kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma kwa siku ya kesho Machi 29, 2025,” ilieleza taarifa hiyo.

Pia, Nguma alisema katika taarifa hiyo kuwa maeneo yatakayokosa maji ni Kiusa, Mawenzi, Bondeni, Njoro Pasua, Bomambuzi, Matindigani, Langoni, Msaranga, Shartours, Kiboriloni, Majengo yote, Mjimpya, Mji mwema, Kwa Mtei, Misitu, KDD, Mjohoroni, Sasaya na Sango.

“Tunaomba wateja wetu wa maeneo yaliyotajwa kuchota maji ya kutosha kwa ajili ya matumizi wakati matengenezo yakiwa yanafanyika, tunaomba radhi kwa changamoto iliyojitokeza,” ilieleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, kutokana na shughuli ya uchimbaji wa lami bado unaendelea ili kulifikia bomba hilo, shughuli ya usitishwaji wa huduma ya maji katika maeneo hayo haukufanyika leo hadi hapo kesho.

Akizungumza na Mwananchi leo, Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando amesema wamechukua jukumu la kufunga barabara hiyo ili kuruhusu matengenezo ya bomba hilo kuendelea.

Amesema magari makubwa yenye uzito wa zaidi ya tani 10 yanashauriwa kutumia barabara mbadala ya Lucy Lameck – Ghaha – Viwanda – Manyema – Mafuta – Nyerere – Bonite – Khambaita. 

Kwa upande wa magari madogo, madereva watatakiwa kutumia barabara ya YMCA – Kilimanjaro kupitia Bustani Alley.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *