Trafiki mbaroni kushiriki kuchota mafuta ajali ya lori

Tabora. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia askari wa usalama barabarani wilaya ya Igunga baada ya kuonekana kwenye picha mjongeo akiwa katikati ya wananchi, waliokuwa wakichota mafuta katika ajali ya lori la mafuta iliyotokea wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema askari huyo, WP 8032 PC Victoria, aliwahi kufika eneo la tukio lakini hakuchukua hatua yoyote kwa watu waliokuwa wakichota mafuta katika ajali hiyo, badala yake alionekana kushiriki kwa kutoa dumu kwa raia ili akinge mafuta.

“Askari huyu hajazingatia taratibu na maadili ya kazi yetu kwa sababu badala ya kuonya wananchi, yeye anashiriki,” amesema Kamanda Abwao.

Kamanda amesema ajali hiyo imetokea Machi 28, 2025, katika Kijiji cha Igogo kwenye barabara kuu ya Igunga-Nzega wilaya ya Igunga, kutokana na uzembe wa dereva wa lori lililokuwa na shehena ya mafuta ya dizeli kugonga kwa nyuma lori lililokuwa limebeba mahindi na baadaye kupoteza uelekeo na kugonga lori jingine ambalo halikuwa na mzigo wowote.

Katika matukio mengine Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora  katika operesheni yake limekamata watuhumiwa 67 wa makosa mbalimbali ambapo jumla ya watuhumiwa watatu  wamepatikana na noti bandia, limekamata watuhumiwa watatu wa kosa la wizi wa pikipiki mbili aina ya San LG moja ikiwa imetolewa namba za usajili.

“Katika nyakati tofauti watuhumiwa wamekutwa na noti hizo bandia na walikua wakija Tabora mjini ili waziweke kwenye mzunguko” amebainisha

Katika hatua nyingine jeshi hilo limekamata watuhumiwa 11 wakiwa na lita 128 za pombe ya moshi na mitambo mitatu ya kutengenezea pombe hiyo huku watuhumiwa 14 wakikamatwa na kilo 13 na gramu 653 za bangi.

Kamanda amesema katika operesheni hizo wamekamata watuhumiwa wengine wanne wakiwa na smagobole matatu yaliyotengenezwa kienyeji na risasi moja.

Kwa upande wa usalama barabarani, amesema imefanyika operesheni na  imetolewa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wa vyombo vya moto 30,614 ambapo madereva wanane wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungiwa leseni.

Pamoja na hayo kumekua na makosa 40 ya unyanyasaji wa kijinsia yaulawiti, kubaka, kutelekeza familia na shambulio yaliyoripotiwa vituoni, ambapo makosa 17 yamefikishwa mahakamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *