
Kila ifikapo Machi 24 huwa ni siku ya kimataifa ya Kifua Kikuu Duniani.
Ni ugonjwa hatari unaoshambulia mapafu na maeneo mengine ya mwili.
Siku hii iliyoadhimishwa Jumatatu wiki hii ilikuwa na kaulimbiu isemayo: “Ndiyo! Tunaweza Kutokomeza kifua kikuu: Kujitolea, Kuwekeza na Kutekeleza.”
Kampeni hii iliyosisitizwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, ilisema kuwa ipo haja ya kuendelea na juhudi za mapambano ya kutokomeza ugonjwa huu licha ya changamoto za kifedha.
Mnamo 2023, ilikadiriwa watu milioni 10.8 waliugua TB ulimwenguni kote, wakiwemo wanaume milioni 6.0, wanawake milioni 3.6 na watoto milioni 1.3. Ugonjwa huu uko katika nchi zote na unaathiri makundi yote.
Karibu robo ya idadi ya watu duniani wameambukizwa na bakteria wa kifua kikuu. Hata hivyo, ni sehemu ndogo tu ya walioambukizwa watakuwa wagonjwa wa kifua kikuu kikali.
Walio na kinga dhaifu ndio wapo katika hatari zaidi ya kuugua. Anayeishi na VVU ana uwezekano wa mara 13 zaidi kupata TB .
WHO imetoa wito wa dharura wa uwekezaji wa rasilimali, lengo likiwa kusaidia huduma za matibabu na msaada kwa wagonjwa wa kifua kikuu.
Ugonjwa huu mara nyingi huwa sambamba na wagonjwa walio na maambukizi ya VVU, kutokana na kujitokeza pale kinga ya mwili inaposhuka.
Ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa unaosababishwa na bakteria wajulikanao kitabibu kama Mycobacteria Tuberculosis.
Mtu mwenye ugonjwa huu mkali katika mapafu anaweza kukohoa mara kwa mara au kipiga chafya, hivyo kuweza kueneza ugonjwa huu kwa njia ya hewa yenye matone madogo yenye maambukizi.
Ili kupunguza hatari zaidi ya ugonjwa huu, ni muhimu kuishi katika makazi yasiyo na msongamano, nyumba zenye madirisha mapana ya kuingiza hewa na mwanga wa jua.
Ukweli wa kisayansi unadhihirisha kuwa vijidudu vya TB hushindwa kuwa hai katika sehemu yenye mazingira ya mwanga wa jua.
Kupata chanjo ya Bacille Calmette-Guérin (BCG), hasa katika nchi zilizo na matukio mengi ya TB. Muhimu wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungua katika huduma za Afya.
BCG ndio chanjo pekee yenye leseni ya kuzuia aina kali za TB kwa watoto, lakini ufanisi wake katika kuzuia TB kwa watu wazima ni mdogo.
Hatua nyingine za kuzuia ni pamoja na watu walio na vihatarishi vingi, ikiwamo wanaoishi na VVU, wazee na watoto kuepuka kuchangamana na wagonjwa wa TB.
Watu walio na maambukizo ya TB iliyofichika wanaweza kupata matibabu ili kuzuia hatari ya kupata TB hai.
Njia nyingine ni kuzuia pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kutopeana mikono, na kuepuka kugusana na watu wenye TB kali wakati wa wiki tatu za kwanza.
Ili kufanikiwa juhudi zianzie katika familia. Muhimu kuwahi kufika kwenye huduma za afya mapema hasa unapopata dalili kama kukohoa kwa zaidi ya wiki mbili.