
London. Ushiriki wa Chelsea na Manchester City katika Fainali za Kombe la Dunia la Klabu ambazo zitafanyika Marekani baadaye mwaka huu umesababisha Ligi Kuu ya England (EPL) kuamua kuwa na madirisha mawili ya usajili katika majira ya kiangazi tofauti na hapo awali ambapo kulikuwa na dirisha moja tu.
Uamuzi wa kuwa na madirisha mawili ya usajili wakati wa majira ya kiangazi unalenga kuziwezesha Machester City na Chelsea kuwahi muda wa usajili wa wachezaji ambao zitawatumia katika Fainali za Kombe la Dunia la Klabu zitakazofanyika kuanzia Juni 14 hadi Julai 13.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao kilichohusisha watendaji wakuu wa klabu zinazoshiriki EPL na Bodi ya Ligi Kuu England, dirisha la kwanza la usajili katika majira ya kiangazi mwaka huu litafunguliwa Juni Mosi na litafungwa Juni 10 ambapo klabu zitaruhusiwa kusajili wachezaji.
Kikao hicho ambacho kimeketi jana jijini London, kimeamua kwamba baada ya hapo, dirisha lingine litafunguliwa kuanzia Juni 16 na kufungwa Septemba Mosi mwaka huu.
Wakati mashindano hayo ya Kombe la Dunia la Klabu yakiendelea, timu pia zitaruhusiwa kuongeza wachezaji wawili kuanzia Juni 27 hadi Julai 3.
Uamuzi wa dirisha la pili la usajili wa majira ya kiangazi mwaka huu kufungwa Septemba Mosi unatajwa kwamba ulipokelewa kwa hisia tofauti kwani awali kulikuwa na mapendekezo kwamba dirisha la usajili lifungwe kabla ya msimu mpya kuanza.
Hata hivyo imeamriwa kwamba tarehe ya kufungwa ibakie Septemba Mosi kwani likifungwa kabla ya msimu kuanza, linaweza kuathiriwa na kuchelewa kufungwa kwa madirisha ya usajili ya ligi nyingine kama Italia, Ujerumani na Saudi Arabia.
Hii n mara ya kwanza katika historia, kuchezwa kwa mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu kwani awali kulikuwepo na mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia ambayo hayakuwa yakishirikisha idadi kubwa ya timu.
Timu 32 zitakazoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu mwaka huu ni Palmeiras, Porto, Al Ahly, Inter Miami, Paris Saint-Germain, Atlético Madrid, Botafogo, Seattle Sounders, Bayern München, Auckland City, Boca Juniors, Benfica, Flamengo, Espérance Sportive de Tunis, Chelsea na Club León.
Nyingine ni River Plate, Urawa Red Diamonds, CF Monterrey , Inter Milan, Fluminense, Borussia Dortmund, Ulsan HD, Mamelodi Sundowns , Manchester City, Wydad AC, Al Ain, Juventus , Real Madrid, Al Hilal, Pachuca, FC Salzburg