Kuna vita ya top four Ligi Kuu

Ligi Kuu Tanzania Bara imebakiza michezo saba ili iweze kumalizika na itapigwa ndani ya miezi miwili, Aprili na Mei baada ya ligi kurejea kutoka kwenye mapumziko.

Hii ni msimu ambao kila timu inaonekana kujipanga vyema na bado kuna vita kuwa ya kuwania ubingwa ambayo inawaniwa na Yanga, Simba na Azam.

Ukiachana na vita hiyo, mwezi ujao utashuhudia mpambano mwingine mkali wa timu gani inaweza kumaliza kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.

Nafasi hii imekuwa maarufu kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na kutoa mwakilishi wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kama bingwa wa Kombe la FA atatoka kwenye zile tatu za juu.

Hivyo, hapa kuna vita kubwa kati ya Singida ambayo inashikilia nafasi hiyo kwa sasa pamoja na Tabora United ambayo imeikalia kooni ikiwa nafasi ya tano.

Singida ambayo ilianza msimu kwa kasi kubwa na kupewa hata nafasi ya kutwaa ubingwa imefanikiwa kukusanya pointi 44, baada ya kucheza michezo 23.

TOP 01

Hata hivyo, haipo sehemu salama sana kwa kuwa ipo mbele ya Tabora kwa pointi saba tu, timu hiyo ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja ikiwa na pointi 37 na kujihakikisha moja kwa moja kubaki kwenye ligi msimu huu.

Hii inaonyesha kuwa kutakuwa na vita kubwa kwenye michezo saba iliyobaki ambayo itatoa picha ya kikosi gani kinaweza kupanda ndege baada ya msimu huu kumalizika.

Michezo saba iliyobaki ina jumla ya pointi 21, hivyo itawalazimu Tabora kuwaombea mabaya wapinzani wao wapoteze angalau michezo mitatu kati ya hiyo nao washinde yote.

Takwimu zinaonyesha kuwa Tabora imebakiza michezo miwili tu nyumbani dhidi ya KMC pamoja na Yanga, lakini wapinzani wao Singida wakiwa na michezo mitatu nyumbani, ambapo watavaana na Kagera Sugar, Prisons na mechi moja ambayo itakuwa ya muhimu kwao wote ni ile ambayo watakutana pamoja ukiwa ni mchezo wa nne kati ya saba iliyobaki.

TOP 02

Hali hii inaonekana kuwa na faida kubwa kwa Singida kwa kuwa imekuwa na kiwango bora kwenye michezo iliyocheza nyumbani.

Takwimu za nyumbani

Timu zote mbili zimeonekana kuwa vizuri kwenye michezo ya nyumbani ambapo kila moja imeshinda sita kati ya 12.

Faida kubwa wanayo Singida kwa kuwa wameonekana kuwa bora zaidi kwani wameshinda sita, wametoka sare minne na kupoteza miwili.

Kwenye eneo la ushambuliaji wamekuwa vizuri kwa kuwa wamefunga mabao  18, wakiruhusu kumi tu.

TOP 03

Kwa upande wa Tabora kwenye michezo 13 waliyocheza nyumbani, wameshinda sita sawa na wapinzani wao, wametoka sare minne na kupoteza mitatu, wakifanikiwa kufunga mabao 27 na kuruhusu 28.

Timu zote mbili zimefanikiwa kukusanya pointi 22 nyumbani hadi sasa ikionekana kuwa ni sehemu ambayo imewafanya kuwa hapo walipo.

Kiwango cha sasa

Hata hivyo, Tabora inaonekana kuwa na wakati ngumu sana kwenye michezo ya hivi karibuni baada ya kushinda mchezo mmoja tu kati ya mitano iliyopita hali ambayo inatishia kasi yao.

Katika michezo hiyo Tabora imetoka sare mitatu na kupoteza mmoja, ambapo kwenye michezo hiyo timu hiyo imefunga mabao manne na kuruhusu manne.

TOP 04

Hali hiyo ni tofauti kwa wapinzani wao Singida ambao kwenye michezo hiyo mitano ya hivi karibuni wameshinda mitatu, wametoka sare mmoja na kupoteza mmoja, ikionekana kuwa moja kati ya timu tatu za juu ambazo zimefanya vizuri zaidi kwenye michezo mitano iliyopita baada ya kuruhusu mabao nane na kuruhusu manne.

Kuvaana na vigogo

Katika michezo iliyobaki Tabora watakutana na kigogo mmoja tu ambaye ni Simba, wakiwa ugenini, lakini hali haiwezi kuwa nzuri sana kwa wapinzani wao Singida ambao watakuwa na pointi sita ngumu dhidi ya timu mbili ambazo wamezifunga kwenye michezo ya kwanza, watakuwa na mchezo dhidi ya Yanga nyumbani na Azam FC ambao wanawania ubingwa wa ligi msimu huu.

Hii ni dhahiri kuwa timu itakayochanga karata zake vizuri ndiyo itamaliza kwenye nne bora msimu huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *