Othman asisitiza amani, utulivu kwenye uchaguzi

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amewaomba Wazanzibari kuomba dua kwa ajili ya amani na utulivu wakati nchi inajiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.

Othman ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo, ametoa wito huo leo Jumatatu Machi 24, 2025  alipohitimisha ziara yake ya mikoa mitano ya Unguja na Pemba.

Othman ambaye alitembelea wagonjwa na wazee, amesema amani ni msingi wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi na salama, huku akitaka wananchi kuhakikisha hakuna vurugu wala machafuko yatakayohatarisha utulivu wa nchi.

“Ndugu zangu, tunapokaribia uchaguzi mkuu Oktoba, nawaomba kila mmoja kwa nafasi yake auombee dua ili tuvuke salama na kwa amani. Tunahitaji uchaguzi wa haki, bila vurugu na bila kuvunja amani ya nchi yetu. Hii ni muhimu ili tuweze kuchagua viongozi bora na sahihi,” amesema Othman.

Othman amesisitiza kuwa, amani itasaidia wananchi kupata nafasi nzuri ya kuwachagua viongozi wanaowataka, lakini ameonya kuvunjika kwa amani kutasababisha athari kubwa, na hata viongozi watakaopatikana katika mazingira ya vurugu, hawataweza kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Katika ziara hiyo, Othman pia amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kujitahidi kuwa karibu na wananchi ili kuwaelewa vyema changamoto zao na kutafuta njia za pamoja za kuzitatua.

Amesema ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni muhimu katika kujenga jamii yenye maendeleo na ustawi.

“Katika kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ni muhimu jamii na waumini kuwa na mshikamano. Wenye nacho wanapaswa kuwasaidia wasiokuwa nacho. Kuongoza ni kujali shida za wananchi, hasa masikini na wale wanaokabiliwa na dhiki na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao,” amesema Othman.

Makamu huyo wa Rais pia, amesema viongozi wanapaswa kuchukua hatua za kusaidia jamii, hasa kwa kuhakikisha matatizo ambayo hayawezi kutatuliwa katika ngazi ya chini, yanapewa kipaumbele ili kutafuta suluhisho katika ngazi za juu.

Katibu wa Mkoa wa Mjini wa ACT-Wazalendo, Mamoud Ali Mahinda amesema ziara ya kutembelea wagonjwa ni sehemu muhimu ya utamaduni wa viongozi, akiongeza kuwa ni hatua yenye manufaa makubwa kwa jamii na Taifa.

Amesema kitendo hicho ni cha kuigwa kutokana na mafundisho ya viongozi waliotangulia.

Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi, Pavu Juma Abdalla amesema ziara hiyo iliyoanzia Pemba hadi Unguja, imewapa viongozi fursa ya kushuhudia matatizo ya kijamii, miundombinu, na changamoto nyingine zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.

Amesema Othman amejionea hali halisi ya wananchi na kuahidi kuwa, wataendelea kushirikiana na jamii kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *