Serikali yaanza kampeni elimu kujikinga na ugonjwa wa Mpox

Rukwa/Dar.  Katika kuhakikisha Jamii inakua salama dhidi ya magonjwa ya mlipuko, Wizara ya Afya imeanza kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya umma na vyombo vya habari kupitia waganga wakuu wa mikoa na wataalamu wa afya.

Hatua hiyo imekuja zikiwa zimepita siku 14 tangu Serikali ilipotangaza kuwa watu wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox. Hii ni mara ya kwanza ugonjwa wa Mpox kuingia nchini.

Akizungumza na Mwananchi leo Machi 24, 2025 Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dk Erasto Silvanus amesema tayari takwimu za maambukizi zimeandaliwa na zitatolewa kwa umma hivi karibuni.

Amesema sampuli za wahisiwa zimeendelea kuchukuliwa na kinachofanyika sasa ni kuhakikisha elimu zaidi inatolewa ili Watanzania wajue namna ya kujikinga.

“Waganga wakuu wa mikoa wanaendelea kutoa elimu kwa kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya kijamii, katika masoko, makanisani  na mwamko ni mkubwa. Tunahamasisha wananchi wakihisi homa wafike kituo cha afya si lazima kusubiri mpaka waone vipele mwilini,” amesema Erasto.

Katika hatua nyingine, wataalamu wa afya ya msingi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wametoa elimu kuhusu ugonjwa huo na jinsi ya kujikinga kwa wafanyabiashara na maofisa usafirishaji.

Akizungumzia hatua hiyo,  Mratibu wa huduma za afya Manispaa ya Sumbawanga, Dk Salum Jipemba amewataka maofisa usafirishaji (bodaboda) kuchukua tahadhari kwa kuwa wao ndio wanakutana na watu wengi.

Dk Jipemba amesema kuwa ili kujikinga na ugonjwa huo ni muhimu maofisa hao wakazingatia kanuni za usafi.

“Kwenye vyombo vyenu hakikisheni kuna vitakasa mikono na maji vitakavyowasaidia abiria kunawa mikono na kubaki salama kwa kuwa mzunguko wa pesa ni mkubwa, sambamba na mwingiliano wa watu tofauti wanaowabeba,” amefafanua Dk Jipemba.

Akieleza dalili za ugonjwa huo, Dk Jipemba amesema ni kupata vipele vinavyotoa maji ambayo mtu mwingine akiguswa na maji hayo anapata maambukizi ya ugonjwa huo.

“Dalili za ugonjwa huo ni homa, maumivu ya kichwa, misuli na mgongo, uchovu wa mwili, kuvimba mitoki ya mwili na vidonda vya koo.”

“Ugonjwa huo unasambazwa kwa njia mbalimbali kama kula au kugusa mizoga ya wanyama pori walioambukizwa wakiwamo nyani, tumbili, sokwe na swala wa misituni.

“Pia mtu anaweza kupata maambukizi kwa kugusa vitu alivyotumia mgonjwa, kugusa majimaji ya mwili na kujamiiana na mtu mwenye maambukizi ya Mpox,” amefafanua.

Amesisitiza kuwa wananchi waache mazoea ya kuchangia vifaa mbalimbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bajaji manispaa ya Sumbawanga, Clement Makundi amesema watahakikisha wanakua na vitakasa mikono, kuacha kushikana mikono, kunawa kila mara, kuepuka kukumbatiana sambamba na kuwa walimu kwa wengine kuhusiana na ugonjwa huo.

“Tutazingatia tahadhari zote tulizopewa ili tusipate maambukizi kwa kuwa sisi tunakutana na watu wengi, tunapokea pesa bila kujua imetoka kwa mtu ambaye ni salama au la!”

Stephano Nicholaus amesema elimu ni muhimu hasa kwa kuweka mabango na kugawa vipeperushi ambavyo  vitasaidia jamii kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya Mpox.

“Kila mmoja azingatie kanuni za afya na kuacha utamaduni wa kupeana mikono,” amesema Stephano.

Machi 7, 2025, Wizara ya Afya kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili.

Dalili hizo ziliambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo

“Kati ya wahisiwa hao, mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam. Baada ya kupokea taarifa za wahisiwa, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa kwa uchunguzi.

“Machi 9, uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwa wahisiwa wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox,” alisema Waziri wa Afya, Jenista Mhagama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *