
Mtwara. Baada ya kesi ya mauaji ya mfanyabiashara na mchimba madini Mussa Hamis, inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara kusimama kwa zaidi ya mwaka mmoja, sasa kesi hiyo inatarajiwa kuanza kuunguruma tena kuanzia leo, Jumatatu, Machi 24, 2025.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Charles Maurice Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelejensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi, Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi, John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa zahanati ya Polisi Mtwara, Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.
Wanadaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis, Januari 5, 2022 katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, na kwenda kuutupa mwili wake katika kijiji cha Majengo, Kata ya Hiari karibu na kiwanda cha saruji cha Dangote.
Wanadaiwa kumuua kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambara, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi, ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizozichukua walipokwenda kumpekua nyumbani kwake, kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea, Lindi, wakimtuhumu wizi wa pesa na pikipiki.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashitaka.
Kikao cha kwanza cha usikilizwaji wa kesi hiyo kilianza Novemba 13 mpaka Desemba Mosi, 2023, ambapo Mahakama ilipokea ushahidi wa mashahidi 10, ambapo Jaji Kakolaki aliahirisha kusubiri kikao kingine.
Hata hivyo tangu wakati huo kesi hiyo haikuwahi kusikilizwa tena mpaka leo ikiwa imetimiza mwaka mmoja, miezi mitatu na siku 22, licha ya vikao mbalimbali vya usikilizwaji wa kesi kama hizo vilivyopangwa katika kipindi hicho katika Masjala mbalimbali za Mahakama Kuu nchini.
Ukimya huo uliwafanya baadhi ya wadau wanaoifuatilia kesi hiyo waliowasiliana na Mwananchi moja kwa moja na wengine katika mitandao ya kijamii kuanza kuiulizia mara kwa mara, huku wengine wakijenga hisia kuwa pengine ilikuwa imeshafutwa kimyakimya.
Hata hivyo Februari 11, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Seraphine Nsaro alilieleza Mwananchi kuwa kesi hiyo ilikuwa bado haijafutwa, huku akibainisha kuwa imechukua muda mrefu kiasi hicho kuendelea kutokana changamoto za ratiba ya utendaji kazi iliyojitokeza.
Hivyo alisisitiza kuwa walikuwa mbioni kuipangia tarehe.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ignas Mwinuka amelithibitishia Mwananchi kuendelea kwa kesi hiyo leo.
“Tayari imeshapangiwa tarehe, imepangwa kuanza leo na kuendelea mfululizo kwa wiki tatu. Tayari nipo Mtwara”, amesema Wakili Mwinuka baada ya kuulizwa na Mwananchi kwenye simu.
Mashahidi waliokwishakutoa ushahidi
Kati ya mashahidi hao 10 waliotoa ushahidi ni shahidi wa kwanza Hawa Bakari ambaye ni mama wa marehemu, ambaye pamoja na maelezo yake aliomba akabidhiwe mifupa ya mwanaye, iliyookotwa mahali alikotupwa baada ya kuuawa ili akaizike.
Shahidi mwingine Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC), wa Ilala Kanda Maalumu Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Yustino Mgonja.
Kamanda Mgonja ambaye wakati wa mauaji hayo alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mtwara, aliieleza Mahakama jinsi kile alichodai mipango ya mauaji hayo ilivyofanyika na kutekelezwa, hatua kwa hatua.
Alidai kuwa aliyafahamu hayo yote kutoka kwa mmoja wa askari hao ambaye pia alikuwa mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo, alipomuhoji ambapo aliwapeleka polisi mahali mwili huo ulikotupwa na ikapatikana mifupa yake ya miguu na mbavu.
Hata hivyo askari huyo alifariki siku chache tu akiwa mahabusu akidaiwa kuwa alijinyonga.
Pia kuna Mkemia wa Serikali Mwandamizi, kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), makao makuu Dar es Salaam, Fidelis Bugoye
Bugoye ambaye ni shahidi wa tisa ndiye aliyefanya uchunguzi wa vinasaba vya mifupa hiyo iliyopatikana mahali ambako mwili wake ulitupwa baada ya kuuawa; na kulinganisha na vinasaba kwenye sampuli ya mate ya mama wa marehemu Mussa, Hawa Bakari Ally ambavyo vilioana.
Shahidi wa 10 na wa mwisho katika kikao hicho cha kwanza alikuwa ni mtunza vielelezo ofisi ya GCLA.
Baada ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, kiongozi wa jopo la waendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Maternus Marandu aliiomba Mahakama iamuru mifupa hiyo ihifadhiwe mahali ambako ni salama kusubiri kikao kingine cha usikilizwaji wa kesi hiyo kitakapopangwa.
Mifupa hiyo ambayo ni mbavu nane, mifupa ya mguu na pamoja suruali ya marehemu, ilipokewa mahakamani hapo Novemba 29, 2023 kupitia shahidi wa tisa wa upande wa mashitaka na kuwa vielelezo vya upande wa mashitaka katika kesi hiyo.
Wakili Marandu alisema kuwa ingawa shahidi wa kwanza ( mama wa marehemu) aliomba akabidhiwe, lakini kwa ajili ya kutenda haki kwa kuwa kesi bado inaendelea ni vema ihifadhiwe kwanza mpaka kesi itakapoisha.
Alisema kuwa kwa kuwa vielelezo hivyo ni mabaki ya viungo vya binadamu vinapaswa kuhifadhiwa mahali maalumu wakati kesi hiyo itakapokuwa inaendelea mpaka hapo Mahakama itakapotoa maelekezo mengine.
Alipendekeza kuwa mahali sahihi ni ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu aliunga mkono kuwa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni mahali sahihi pa kuhifadhi vielelezo hivyo.
Mahakama ilikubaliana na maombi na hoja na mapendekezo ya upande wa mashitaka na inaelekeza mifupa hiyo ihifadhiwe katika hizo Kanda ya Kusini Mtwara.
“Kwa kuwa ni viungo vya binadamu vinahitaji kutunzwa kwa utu na mahali salama”, alisema Jaji Kakolaki na kuongeza:
“Natoa maelekezo viwekwe sehemu salama ambako ni Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kusini Mtwara.