Uzalishaji hewa tiba ya oksijeni utakavyookoa maisha, gharama

Dar es Salaam. Ongezeko la uzalishaji wa oksijeni ya matibabu, kupitia mitambo inayojengwa na Kampuni ya Tanzania Oxygen (TOL) limetajwa litaboresha upatikanaji wake, pamoja na kupunguza gharama kwa asilimia 35 katika hospitali na vituo vya afya nchini.

Machi 20, 2025 wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mitambo ya kuzalisha oksijeni kwa matumizi ya hospitali, ilielezwa mahitaji ya gesi hizo nchini kwa sasa ni makubwa.

Kwa mujibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kwa siku mgonjwa mmoja anaweza kutumia oksijeni ya kati ya Sh30,000 mpaka Sh50,000 ambayo hata hivyo wagonjwa wengi katika hospitali za umma hawatozwi, bali Serikali inagharamia.

“Oksijeni ni hewa tiba muhimu kwenye matibabu, Serikali ilifanya tathmini miaka minne iliyopita na ilionekana tulikuwa tunazalisha asilimia 20 ya mahitaji, kulikuwa na pengo karibu asilimia 78, kumekuwa na jitihada za kuwezesha jitihada za upatikanaji wake,” amesema Rais wa MAT Dk Mugisha Nkoronko.

Wagonjwa wa mfumo wa upumuaji na kifua kikuu ndiyo wahitaji zaidi. Katika matibabu, wapo ambao hulazimika kuishi katika hewa tiba ya oksijeni kwa miezi minane mpaka miaka miwili.

Mwaka 2020 wakati wa janga la Uviko-19 ilionekana kuna uhitaji mkubwa wa oksijeni na uwezo wa wazalishaji wa ndani ulikuwa ni mitungi 1,200 kwa siku ukilinganisha na mahitaji ya zaidi ya mitungi 4,600 kwa siku.

Hata hivyo, Serikali ilianzisha mpango wa kuimarisha upatikanaji wa hewa tiba ya oksijeni kwa kusimika mitambo ya uzalishaji wa hewa tiba takribani 44.

Akiweka jiwe la msingi TOL Gases, Majaliwa amesema mradi huo unaunga mkono juhudi endelevu za Serikali za kuhakikisha oksijeni kwa ajili ya matibabu inapatikana kwa urahisi katika kila kituo cha huduma za afya nchini.

“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na zahanati nchini na kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya kupumua, ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya akina mama na kuokoa ya watoto wa Taifa hili,” amesema Majaliwa.

Pia, amesema mradi huo utakapokamilika utazalisha lita milioni 4.1 za oksijeni ya matibabu kwa mwaka kuanzia mwaka 2026.

“Hatua hii itaboresha upatikanaji wa oksijeni katika hospitali na vituo vya afya, pamoja na kupunguza gharama za oksijeni ya matibabu kwa asilimia 35 katika hospitali na vituo vya afya kote nchini, hivyo kuimarisha huduma za afya kwa wananchi,” amesema Majaliwa.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema mradi huo ni muhimu kwa sababu oksijeni inayozalishwa kwa njia hiyo inakuwa na viwango vya ubora, hivyo itasaidia kuimarisha huduma za afya zitolewazo nchini pamoja na kupunguza vifo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases, Daniel Warungu ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuimarisha na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Mtambo huo wa kuzalisha gesi pamoja na iliyofungwa na Serikali katika hospitali za rufaa, kanda na halmashauri nchini, itasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa hewatiba ya oksijeni na kuokoa fedha za Serikali kwa asilimia 50.

Mhandisi wa vifaa vya matibabu Wizara ya Afya, Suvina Haule amesema awali mtungi mmoja ulikuwa unauzwa kati ya Sh40,000 hadi Sh55,000 kwa sasa utapatikana kwa bei isiyozidi Sh25,000.

“Malengo ilikuwa mpaka Desemba 2024 tufunge mitambo 61. Tulifanya ununuzi wa dharura wa mitambo saba mwaka 2020 ikafungwa mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam (Ilala), Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Geita na Manyara.

“Katika maeneo hayo matarajio ilikuwa kila mkoa uzalishe mitungi 200 ya oksijeni kwa siku. Jukumu jingine ilikuwa mikoa hiyo isambaze kwa mikoa inayoizunguka. Baada ya kukamilika ikaonekana uhitaji wa oksijeni bado ni mkubwa, tuliongeza mitambo mingine 12,” amesema Suniva.

Amesema mitambo hiyo ikafungwa mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma, Simiyu, Musoma, Tabora, Mwanza, Songwe, Lindi na Njombe na halmashauri zisizofikika ikiwamo Buhigwe, Bumbuli, Iramba na Karagwe.

Suniva amesema awamu nyingine ilifikishwa mitambo 25 iliyogawanywa hospitali za rufaa ambazo zilikuwa hazijapata ikiwamo Kibong’oto, Muhimbili, JKCI, MOI, Mtwara, Mbeya na META na halmshauri kadhaa.

Gharama kupungua

Kwa mujibu wa wataalamu wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji nchini, oksijeni tiba ina gharama, hivyo wengi hushindwa kumudu gharama.

Hata hivyo, wamesema ongezeko la wazalishaji wa oksijeni tiba nchini litasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza gharama hiyo.

“Wakati wa mlipuko wa Uviko-19 oksijeni ilituishia, kwa kuwa hospitali nyingi zilikuwa hazina mashine za kutengenezea oksijeni, ilitupatia changamoto tukaanza kutengeneza wenyewe ile ilisaidia sana,” amesema daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji Aga Khan, Alex Masao.

Amesema kwa Tanzania kuwa na mitambo kwa sasa, itasaidia kupunguza gharama kubwa ambayo wagonjwa na ndugu wamekuwa wakitumia fedha nyingi pindi mgonjwa anapolazimika kuingizwa kwenye oksijeni tiba.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elisha Osati alitolea mfano kwa mgonjwa aliyepo ICU anayelazimika kutumia oksijeni kwa saa 24 hulipia Sh500,000 kwa jumla.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa oksijeni tiba kwa kuwa uhitaji ni mkubwa.

“Mara nyingi kwenye hospitali za chini, mgonjwa anapewa rufaa kuja huku juu kwa sababu oksijeni hakuna, analetwa na gari ya wagonjwa na mtungi mmoja wa oksijeni analetwa Muhimbili, kwa kuwa oksijeni inapatikana,” amesema.

Dk Osati amesema baada ya Muhimbili kujenga mashine ya kuzalisha oksijeni ilisaidia upatikanaji kwa kiasi kikubwa na wakati huo pia hospitali za rufaa za mikoa zilijenga.

Amesema mahitaji zaidi ya oksijeni hiyo ni pale yanapotokea magonjwa ya milipuko, yanayohitaji kumlaza mgonjwa ICU au HDU.

Dk Osati amewataja wagonjwa wenye matatizo ya moyo, mapafu, figo, pumu, upungufu mkubwa wa damu au nimonia kuwa mara nyingi ndio huhitaji zaidi huduma za oksijeni.

Dk Nkoronko amesema ni muhimu nchi kuachana na utaratibu wa kutumia mitungi, kwani licha ya kwamba unawasumbua watumishi kuubeba, kuufungua, kumwekea mgonjwa hauna ufanisi wa kutosha kwa kila wodi na kwamba oksijeni ya kuzambaza kupitia bomba ni muhimu zaidi.

“Tunatamani hospitali zijengewe uwezo kuzalisha oksijeni yake ili ifike Mwanza, kwa staili ya sasa itafika nusu, nyingi utapotea njiani sababu ya joto. Tunatamani tuondoe adha ya mitungi kupitia mabomba ya kusambaza oksijeni wodini.

“Kuzalisha au kuhifadhi mtandao wa mabomba uliowekwa chanzo cha uzalishaji, mpaka kumfikia mgonjwa ndiyo tiba nzuri zaidi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *