Dar es Salaam. Baada ya Darassa kuachia albamu yake ya pili, Take Away The Pain (2025), naye Lady Jaydee ameweka wazi kuwa Juni atatoa albamu ambayo itakuwa ya 10 kwake ikienda sambamba na kuadhimisha miaka yake 25 katika Bongo Fleva.
Inatarajiwa hadi utakapomalizika mwaka 2025 wasanii wakubwa wa Bongo Fleva zaidi ya 10 watakuwa wametoa albamu, tayari majina makubwa kama Diamond Platnumz, Nandy, Harmonize na Jay Melody yameweka wazi ujio wa albamu zao kwa mwaka huu.
Kwa miaka zaidi ya tano sasa, imeshuhudiwa wasanii zaidi ya 15 kila mwaka wakitoa albamu katika mfumo wa kidijitali ambao ni soko jipya linalokuwa kwa kasi lakini wasanii wanalilinda vipi?.

Hakuna ubishi kuwa kuimarika kwa soko la muziki mtandaoni nchini kumechochea hilo kwa kiwango kikubwa, hatua hiyo imepelekea kampuni za kimataifa zinazojishughulisha na kuuza na kusambaza muziki kuingia makubaliano ya ushirikiano na wasanii wengi.
Soko la kidijitali limekuwa mkombozi baada ya wasanii kuachana kabisa na utamaduni wa kutoa albamu katika mfumo wa nakala halisi (kanda) kutokana na ushamiri kwa uharamia kwenye soko ambapo wajanja wachache walijinufaisha kupitia kazi hizo.
Hata hivyo, wizi bado upo kwa kiasi chake huko mitaani ila katika soko la mtandao ambalo ndilo hasa wasanii wanalilenga, suala la hakimiliki linaheshika na kulindwa kidijitali na kampuni ambazo wasanii huwapa kazi ya kusambaza muziki wao.
Uzuri wa sasa au dijitali, msanii mwenyewe ana uwezo wa kufuatilia na kujua kazi yake imeuzika kwa watu wangapi na kwa muda gani na kukadiria kiwango cha mapato aliyoingiza tofauti na kipindi cha kuuza kanda kwenye maduka ya watu binafsi.
Wakati biashara hii inazidi kukua kwa kuwavutia wateja wengi, ni wakati mwafaka kwa wasanii wa Bongo Fleva kutengeneza misingi ya kuilinda na ili soko lake liendelee kuwepo na kuufikisha muziki wao mbali na wao kunufaika zaidi.

Je, ni kwa namna gani wanaweza kufanikiwa katika hilo?, mambo haya matatu yanaweza kuwa na mchango mkubwa kufanikisha mpango huo.
Mosi; kutengeneza nyimbo (audio) zenye viwango ambavyo zinakidhi mahitaji yaliyopo katika soko lenye ushindani, hiyo ni kutokana kazi zote za wasanii wote duniani zinauzwa katika jukwaa moja, iwe ni Spotify, Tidal, Boomplay au iTunes Music.
Kwa miaka wasanii wengi Bongo wamekuwa wakitumia fedha nyingi kusafiri huku na kule kwa ajili ya kutengeneza video za nyimbo zao, ila idadi kubwa ya nyimbo zenyewe zikiwa chini ya viwango, yaani unakuta video kali ila audio haisikiliziki.
Hivyo tunaweza kusema wasanii wamewekeza nguvu kubwa upande wa video kuliko audio, hilo halina afya kwa biashara yao ya albamu kwani walaji wengi wa bidhaa yao ni wasikilizaji na sio watazamaji.
Pili; wasanii wanapaswa kuwa na timu ya wataalamu wa kusimamia maudhui yao mtandao ili kuweza kumudu biashara hiyo, ukweli ni kwamba sio kila msanii anayeweka muziki mtandaoni anapata fedha nzuri.
Wanaofanikiwa ni wale ambao wameamua kuwekeza upande huo na kuwaachia watalaamu kufanya kazi yao, kwa hapa Bongo mfano mzuri ni Diamond na WCB Wasafi kwa ujumla ambao wanafanya vizuri katika eneo hilo.
Kutozingatia utaalam ni hasara, mfano albamu ya Harmonize, Afro East (2020) iliwahi kuondolewa Tidal, Amazon Music, Deezer, Yandex na YouTube na kutokana na kunakili wimbo wa Papa Wemba, Show Me the Way (1995) bila kufuata taratibu za hakimiliki.
Mambo kama hayo ni sawa na kupiga hatua 10 mbele na kurudi nane nyuma, msanii anapotoa albamu ndio watu wanakiu ya kuisikiliza, sasa inapotoka na kuondolewa tena sokoni, ni kutoa mwanya kwa wajanja kufanya yao.
Tatu; biashara yoyote ile inahitaji matangazo ili kuweza kuvutia na kushawishi wateja wengi, hivyo hivyo upande wa muziki, wasanii wengi wanaamini kutangaza kupitia vyombo vya habari na kurasa zao za mitandao wa kijamii kuwa wanatoa albamu hiyo inatosha.

Hapana, jitihada zaidi zinahitajika, ingawa kampuni zinazoingia makubuliano na wasanii kwa ajili ya kusambaza kazi zao hufanya hivyo, ila wasanii hawatakiwi kubweteka maana muziki utabaki kuwa wao miaka yote kwani mikataba ya kibiashara hufika ukomo.
Wasanii wa Nigeria wanaonekana kufanikiwa zaidi kimauzo illa ukichunguza utabaini wanafanya kazi na kampuni kubwa za nje kwa ajili ya kutangaza muziki wao na chapa zao. Ndio sababu utaona albamu zao zinachaguliwa kuwania tuzo kubwa kama Grammy na hata kushinda.