
Papa Francis atatoa salamu na baraka kwa sala ya kila wiki ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye dirisha la Hospitali ya Gemelli ya Roma siku ya Jumapili, ikiwa ni mara yake ya kwanza kuonekana hadharani tangu kulazwa hospitalini hapo Februari 14, Vatican imetangaza Jumamosi.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
“Papa Francis anatarajia kutoa salamu na baraka kutoka Hospitali ya Agostino Gemelli huko Roma mwishoni mwa sala ya Malaika wa Bwana, ambayo itawasilishwa kwa njia ya maandishi kama katika wiki za hivi karibuni,” ofisi ya waandishi wa habari ya Vatican imesema.
Papa mwenye umri wa miaka 88 amelazwa hospitalini kwa wiki tano sasa kutokana na homa ya mapafu ambapo katika kipindi hicho Vatican alisikika mara moja tu Machi 6, ambapo sauti yake ilikuwa dhaifu, ilikatika-katika na haikuwa rahisi kueleweka.
Hata hivyo Papa Francis anaendelea kurejesha nguvu zake polepole hospitalini lakini analazimika “kujifunza tena kuzungumza” baada ya matumizi ya muda mrefu ya tiba ya oksijeni yenye mtiririko mkubwa, Kardinali Victor Manuel Fernandez amesema.
Kardinali huyo, ambaye ni mkuu wa ofisi ya mafundisho ya imani ya Vatican, alikanusha uvumi kwamba Papa angejiuzulu na kusema kuwa anarejea katika hali yake ya kawaida.
“Papa yuko vizuri sana, lakini oksijeni yenye mtiririko mkubwa hufanya koo kukauka sana. Anahitaji kujifunza tena jinsi ya kuzungumza, lakini hali yake ya jumla ya mwili iko kama ilivyokuwa hapo awali,”* Fernandez alisema wakati wa uzinduzi wa kitabu kipya cha Papa kuhusu ushairi.
Katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu afya yake iliyotolewa Ijumaa, Vatican ilisema hali ya Papa bado ni tulivu na imeonyesha “maendeleo madogo katika kupumua na kutembea.”
Taarifa hiyo ilithibitisha kuwa tangu Jumatatu, hajatumia mashine ya kusaidia kupumua usiku, bali anapokea oksijeni kupitia kibomba kidogo puani kwa muda mwingi mchana. Bado hakuna taarifa rasmi kuhusu lini atatoka hospitalini na kurejea Vatican, na Fernandez alisema hajui kama Papa ataruhusiwa kabla ya Pasaka, itakayoadhimishwa Aprili 20.