ZIMEBAKI mechi saba za kujitetea kwa timu mbili kuepuka kushuka daraja kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu huku takwimu zikionyesha zina kazi kubwa ya kufanya.
Timu hizo ni zile zinazoshika nafasi ya 16 na 15 ambapo kama msimu ukimalizika zikiendelea kubaki hapo, basi zitashuka moja kwa moja kama ambavyo Kanuni ya 6(2) ya Ligi Kuu Bara inavyeleza kuwa: “Timu mbili (2) za mwisho, zilizoshika nafasi ya 15 na 16 kwenye Ligi Kuu zitashuka moja kwa moja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (Championship) msimu unaofuata.”
Kwa sasa timu zinazoshika nafasi hizo ni KenGold yenye pointi 16 na Tanzania Prisons (18) zinazotokea Mbeya huku pia jiji hilo likiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza timu mbili ndani ya misimu mitatu iliyopita ambapo Mbeya Kwanza ilishuka 2021-2022 na Mbeya City ikashuka 2022-2023.
Mbali na timu hizo, pia zipo Kagera Sugar iliyopo nafasi ya 14 ikikusanya pointi 19 na Pamba Jiji (22) nafasi ya 13 ambazo zipo kwenye mstari wa kucheza playoff kuepuka kushuka daraja.
Wakati timu hizo zikiwa kwenye hatari hiyo, takwimu za misimu mitatu iliyopita zinaonyesha timu zilizoshuka daraja moja kwa moja ni zile zilizoshindwa kufikisha pointi 30.
Hata hivyo, zipo zilizowahi kufikisha pointi hizo lakini zikashuka kupitia mechi za mtoano kama ilivyokuwa Mbeya City msimu wa 2022-2023, huku Tanzania Prisons ikinusurika na janga hilo msimu wa 2021-2022 ilipomaliza ligi na pointi 29, ikaponea katika mechi za mtoano.

Ikiwa ndiyo inashiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu wake wa kwanza, imekuwa haina matokeo mazuri tangu mwanzo ambapo ilimaliza duru la kwanza ikikusanya pointi sita pekee katika mechi 15 ilizocheza, lakini duru la pili iliamka ikicheza mechi nane na kukusanya pointi 10 zinazowafanya hivi sasa kuwa nazo 16 baada ya mechi 23 ikiendelea kubaki mkiani.
Mtihani wa KenGold ni kupambana katika mechi hizo saba zenye pointi 21 ikusanye angalau 15 zitakazowafanya kufikisha 31 ili kujitoa kwenye jinamizi hilo.
Katika kuzisaka pointi hizo 15, ina kibarua cha kukabiliana na timu mbili zilizopo kwenye hatari zaidi ya kushuka kama wao ambazo ni Tanzania Prisons na Pamba Jiji, lakini pia itacheza dhidi ya Simba inayopambana kuusaka ubingwa sambamba na Azam inayopigania kutotoka tatu bora.
Mechi nyingine ni dhidi ya Namungo, Coastal Union na Dodoma Jiji ambazo zote itakuwa ugenini na ukiangalia msimamo wa ligi ulivyo hivi sasa, nazo hazijajihakikishia kubaki bado, zinahitaji kupambana kuwa salama.
Ugumu wa ratiba hiyo unaifanya KenGold kuwa kwenye asilimia kubwa zaidi ya kushindwa kufikisha pointi 30, hivyo moja kwa moja itapitia njia ambazo wenzake wamepitia kwa kushuka daraja na kushiriki Championship.
Katika mechi zake saba zilizobaki kwa KenGold, nne itacheza nyumbani dhidi ya Azam, Tanzania Prisons na Simba Pamba Jiji huku rekodi ya uwanja wake wa nyumbani ikionyesha imekusanya pointi 14 zilizotokana na kushinda mechi tatu sawa na ilizopoteza huku sare zikiwa tano.
Kwa ugenini, rekodi ya KenGold inaonyesha timu hiyo imekusanya pointi mbili pekee huku ikiwa haijashinda mechi yoyote kati ya 12 ilizocheza, hivyo kwa hesabu za harakaharaka nafasi ya kushinda ni ndogo sana.
Ukiangalia wapinzani aliobaki nao katika duru la kwanza walipokutana hakuna hata mechi moja aliyoondoka na ushindi zaidi ya kuambulia sare mbili tena zote nyumbani.
Matokeo ya mechi hizo yapo hivi; Azam (4-1), Dodoma Jiji (2-2), Tanzania Prisons (1-0), Coastal Union (1-1), Pamba Jiji (1-0), Simba (2-0) na Namungo (3-2).
Kutokana na mtihani walionao, Kocha Mkuu wa KenGold, Vladislav Heric, amesema: “Mechi ambazo zinatuumiza kichwa zaidi ni dhidi ya Simba na Azam, unajua hizi ni timu mbili bora kati ya tatu au nne, na unaona na wao wana hesabu zao za kule juu, lakini tuna malengo yetu, hapo kuna pointi tutazitaka kama sio zote basi angalau tatu au nne.
“Hizi mechi zingine tano zilizosalia kwa kikosi tulichonacho, naona tuna nafasi ya kushinda, kitu muhimu ni kuzicheza kama fainali kwetu, nitawaambia wachezaji wangu tutakuwa na kazi ngumu hatutakiwi kuruhusu kushuka daraja.”

TANZANIA PRISONS
Ilinusurika kushuka daraja msimu wa 2021-2022 baada ya ‘playoff’ ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar kupoteza, kisha ikaenda kucheza dhidi ya JKT Tanzania na kushinda.
Kwa sasa hali imekuwa ngumu zaidi kwao, timu hiyo ikiwa imebakiwa na mechi saba za kumaliza msimu huu, nayo inapambana kuepuka mtego wa kutofikisha pointi 30.
Tanzania Prisons inayonolewa na Kocha Aman Josiah, aliyechukua mikoba ya Mbwana Makata aliyeondolewa kikosini hapo mwishoni mwa mwaka jana, kwa sasa inashika nafasi ya 15 ikikusanya pointi 18 huku msimu wa 2021-2022 ambao ilicheza mechi za mtoano ilimaliza ligi na pointi 29.
Ili kufikisha pointi 30, Tanzania Prisons inahitaji kufanya vizuri katika mechi saba dhidi ya KMC (ugenini), Kagera Sugar (nyumbani), KenGold (ugenini), JKT Tanzania (nyumbani), Coastal Union (nyumbani), Yanga (nyumbani) na Singida Black Stars (ugenini).
Katika duru la kwanza, Tanzania Prisons dhidi ya wapinzani aliobaki nao alikusanya pointi nne pekee baada ya kuifunga KenGold na kutoka suluhu dhidi ya Kagera Sugar.
Matokeo yalikuwa hivi; Tanzania Prisons 1-2 KMC, Kagera Sugar 0-0 Tanzania Prisons, Tanzania Prisons 1-0 KenGold, JKT Tanzania 1-0 Tanzania Prisons, Coastal Union 2-1 Tanzania Prisons, Yanga 4-0 Tanzania Prisons na Tanzania Prisons 0-2 Singida Black Stars.
Ukiziweka kando hizo mbili za chini kabisa, Kagera Sugar nayo inaweza kushuka daraja moja kwa moja kufuatia hivi sasa kukusanya pointi 19 katika mechi 23 huku ikiwa haina matokeo mazuri ya mwendelezo kama ilivyo kwa Pamba Jiji iliyopo nafasi ya 13 na pointi 22.
Timu zingine ambazo zina mtihani wa kufikisha pointi 30 kujinasua na rekodi mbaya iliyopo kwa misimu mitatu nyuma ni Fountain Gate (28), Dodoma Jiji (27), Coastal Union (25), Mashujaa (24), KMC (24) na Namungo (23).
MECHI ZA PAMBA JIJI
Tabora United
Fountain Gate
JKT Tanzania
MECHI ZA KAGERA SUGAR
Coastal Union
Tanzania Prisons
Dodoma Jiji
MECHI ZA TANZANIA PRISONS
Kagera Sugar
JKT Tanzania
Coastal Union
Singida Black Stars
MECHI ZA KENGOLD
Dodoma Jiji
Tanzania Prisons
Coastal Union
Pamba Jiji
REKODI ZA MISIMU MITATU ILIYOPITA
P W D L GF GA Pts
13.JKT Tanzania 30 6 14 10 21 30 32
14.Tabora UTD 30 5 12 13 20 41 27
15.Geita Gold 30 5 10 15 18 38 25
16.Mtibwa Sugar 30 5 6 19 30 54 21
P W D L GF GA Pts
13.KMC 30 8 8 14 25 31 32
14.Mbeya City 30 7 10 13 34 44 31
15.Polisi TZ 30 6 7 17 25 54 25
16.Ruvu 30 5 5 20 19 42 20
P W D L GF GA Pts
13.Mtibwa 30 7 10 13 25 34 31
14.Prisons 30 7 8 15 21 34 29
15.Biashara 30 5 13 12 23 35 28
16.Mbeya Kwanza 30 5 10 15 22 39 25