Dar es Salaam. Wakati ukaguzi unaofanywa na trafiki kwa magari ya daladala ukilalamikiwa na baadhi ya wamiliki wakidai wanakomolewa, Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa) umesema huo ni ukaguzi wa kawaida dhidi ya magari mabovu.
Ukaguzi huo ulioanza Jumatano, Machi 19, 2025, kwa kuangalia makosa mbalimbali kwenye magari hayo yanayofanya safari zake Chanika, Kigogo, na Kisarawe, umeanza siku chache baada ya kutokea ajali Machi 17, 2025, katika eneo la Pugu Mwisho wa Lami na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Polisi Chanika, Awadhi Mohamed Chiko. Gari la Awadhi liligongana na daladala, dereva wa daladala hilo alitoweka.
Kwa mujibu wa polisi, ukaguzi huo ni wa kawaida kwa lengo la kudhibiti makosa ya usalama barabarani.
Hata hivyo, Mkuu wa Trafiki Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Boniface Mbao, aliyekuwa kwenye ukaguzi Pugu, alisema ukaguzi huo ni wa kawaida na kutaka maelezo zaidi kutafutwa kwa Mkuu wa Polisi Kanda u ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kwa kuwa ndiye msemaji wa suala hilo.
Muliro alipotafutwa kwa simu yake ya kiganjani, alipokea na kusema yupo kwenye kikao, hivyo atafutwe baadaye, lakini hata alipotafutwa tena, simu yake iliita bila kupokelewa.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema, akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hii, alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa wanachama kuhusu msako wa daladala.
Hata hivyo, Lema alisema ni mapema kutoa tamko la kulalamikia suala hilo, ukizingatia kuwa kinachofanywa ni moja ya majukumu ya polisi wa usalama barabarani.
“Mpaka sasa hatujapokea taarifa ya mtu kubambikiwa makosa katika ukaguzi huo, jambo ambalo kama lingetokea, tungeliingilia kati,” alisema Lema.

Kondakta akiwa anawarudishia abiria nauli zao baada ya kushushwa kwenye gari na Polisi wa kikosi cha Usalama barabarani waliokuwa kwenye ukaguzi wa kawaida eneo la Pugu shule ya Msingi, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Dalaam.
Hata hivyo, aliwasihi wamiliki wa daladala wanaoona magari yao yana matatizo kuyafanyia marekebisho ili kuepuka usumbufu huo.
“Mbona mengine yapo barabarani? Ina maana kama lako limelamatwa, basi kweli lina shida,” alisema Lema.
Kuhusu malalamiko ya chama kutokuwa na msaada kwa wanachama wake, alisema hawawezi kukurupuka bila ya mmiliki mmoja mmoja kuwasilisha malalamiko yake, kwa kuwa kila mtu anakutwa na makosa tofauti.
Pia, alisema haitakuwa sawa kuingilia majukumu ya kikosi cha usalama barabarani kufanya kazi zake bila sababu inayoshikika.
Madereva wa daladala walalamikia ukaguzi
Baadhi ya madereva wa daladala waliozungumza leo kwa nyakati tofauti wamesema ukaguzi huo haijafanyika tu Pugu, bali ni Dar es Salaam yote
Dereva Jumanne Patrick, anayeendesha daladala kati ya kituo cha Simu 2000 na Mnazi Mmoja, amesema kuwa kutokana na msako huo, magari mengi kituoni leo yamepungua.
“Huu msako tangu jana unatutesa kweli. Baadhi ya madereva wameamua kutotoa gari zao leo kwa kuwa inaonekana bado ukaguzi ni shughuli endelevu,” amesema Patrick.
Naye mmiliki wa daladala, Break Salum, amesema kati ya daladala 30 anazomiliki, saba tayari zimekamatwa.
Salum, ambaye magari yake yanahudumu katika njia mbalimbali jijini, amesema kuwa kutokana na hali hiyo, kwa njia ya Mbagala, amelazimika kusimamisha huduma ya usafiri.
Hata hivyo, amesema anaona ukaguzi huo unafanywa kwa nia ya kuwakomoa wamiliki wa daladala kwa kuwa kuna makosa ambayo hayahusiani moja kwa moja na ajali.
“Mfano, gari lina kioo kilichopasuka kidogo, lakini unanig’olea namba eti nikatengeneze, au kitasa cha mlango – vitu ambavyo havihusiani moja kwa moja na ajali.
“Nashauri makosa ya aina hiyo tuandikiwe hata cheti, lakini si kung’olewa namba. Mbali na sisi kuingiza fedha kidogo, trafiki wanapaswa kuelewa kuwa tunatoa huduma kwa wananchi, na tangu jana tumeona wanavyotaabika barabarani,” amesema mmiliki huyo.
Kwa upande wao, abiria wamesema siku hizi mbili zimekuwa ngumu kwao kupata usafiri kutokana na ukaguzi huo.
Elly Mavura, mkazi wa Mbezi, amesema kuwa jana kituo cha daladala Mbezi hakukuwa na magari, na ilimchukua saa mbili kusubiri bila mafanikio, hadi alipoamua kukodi bajaji
“Serikali iangalie inapofanya ukaguzi, kwa sababu sisi wananchi walalahoi tunategemea usafiri huu. Kama ni makosa ambayo mwenye daladala anaweza, huku gari ikiendelea kutoa huduma, apewe muda badala ya kuling’oa namba kabisa,” amesema Mavura
Shinuna Kimweri, mkazi wa Gongolamboto na mfanyabiashara wa samaki, amesema kuwa ameingia gharama za usafiri wa bodaboda baada ya kutokuwepo kwa daladala, ambapo awali alizoea kutumia Sh1,600 kwenda na kurudi, lakini sasa ametumia Sh10,000.
“Kibiashara ni hasara, kwani faida ninayopata kwenye uuzaji wa samaki ni ndogo.
“Wakati ninaingia hasara hizi, wateja wangu wanataka niwauzie kwa bei ileile ya kawaida. Hawaelewi kuwa nimepata gharama kubwa za usafiri,” amesema.