Ni muhimu wasomi kupata ujuzi Veta

Jumanne wiki hii nilihudhuria maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ndiye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.

Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya “Ukuzaji Stadi na Ubunifu kwa Maendeleo ya Jamii na Taifa”, yamekuwa yakifanyika kwa wiki nzima, ambapo kauli ya Waziri Mkuu Majaliwa, kuwa wahitimu wa vyuo vikuu wakasome Veta, imepokewa kwa hisia tofauti, zenye sintofahamu fulani.

Kauli hiyo imepokewa vibaya na wasomi wa vyuo vikuu, wanaoringia usomi wao, hata kama usomi huo hauwasaidii kitu, hivyo kitendo cha kuambiwa wakasome Veta, wanajiona kama wamedharauliwa.

Baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu nao wameipokea vibaya kauli hiyo, kwa kuona Waziri Mkuu, ni kama ametangazia taifa kuwa elimu ya chuo kikuu kwa sasa, ni kama haina maana tena, mambo yote ni elimu ya ufundi stadi inayotolewa na Veta, hivyo kuogopa kuitikiwa kwa wanafunzi badala ya kuomba udahili wa vyuo vikuu, bora waende Veta.

Ukweli utabaki kuwa ukweli, watu wanaoongoza kwa kutegemea ajira za maofisini, ni wasomi wa vyuo vikuu, wanaojiona wao ni wasomi sana, wamesoma sana, na wanastahili kazi za maana, huku wakiwaona wahitimu wa Veta kama ni wale darasa la saba, waliofeli na kushindwa kujiunga sekondari ndio wanategemea Veta.

Juzi pale ukumbini, zilitolewa shuhuda 10 za wahitimu wa vyuo vikuu, waliokosa kazi baada ya kuhitimu, na walipoamua kujiunga Veta kusomea ufundi stadi, sasa ni matajiri wakubwa, siyo tu kwa kujiajiri, bali pia kwa kuajiri wengine.

Ukweli mchungu kuhusu elimu yetu ya chuo kikuu inawafundisha watu kutegemea ajira.

Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alieleza kuwa maadhimisho hayo yamehusisha shughuli mbalimbali, ikiwemo utoaji wa huduma kwa jamii, maonyesho ya teknolojia na ujuzi, pamoja na utoaji wa tuzo na vyeti vya heshima kwa watu waliotatua changamoto za maendeleo ya ufundi stadi nchini.

Veta, ambayo ilianzishwa mwaka 1994 kwa Sheria ya Bunge na kuanza kazi rasmi mwaka 1995, imeendelea kuwa muhimu katika kuwajengea Watanzania uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa, na pia kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Pia, imejizatiti katika kutoa elimu ya ufundi katika sekta mbalimbali, kama vile viwanda, kilimo, ujenzi, teknolojia, nishati, huduma na utalii.

Maadhimisho haya ya miaka 30 ya Veta, yanatokea wakati ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan ameagiza kukamilika kwa ujenzi wa vyuo vya Veta vya hadhi ya kimkoa katika mikoa ambayo haikuwa na vyuo hivyo, na kujenga vyuo vya Veta vyenye hadhi ya kiwilaya katika wilaya zote nchini Tanzania ambazo hazikuwa na vyuo vya aina hiyo.

Hivi sasa, ujenzi wa chuo cha Veta cha Mkoa wa Songwe unaendelea, na ujenzi wa vyuo vingine 64 katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazina vyuo unakamilika. Haya ni maendeleo makubwa sana kwa awamu hii ya 6 na Watanzania tukubali, tukatae, huyu mama anastahili kupewa maua yake na kama maua stahiki kwake ni mitano tena, mimi nasema, apewe tu!

Waziri Mkenda alitoa wito kwa vyuo vya Veta na wananchi kushiriki kwa wingi katika maadhimisho haya, hususan kilele chake mjini Dar es Salaam, ili kujadili umuhimu wa elimu na ujuzi katika maendeleo ya taifa, kulingana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023.

Lakini juzi kwenye amsha amsha iliyofanyika kwenye ukumbi wa jengo la PSSSF Golden Jubilee Hall, DSM, mdau wa sekta ya nguo na mavazi wa Kitanzania, Waziri Profesa Mkenda kwanza alitangaza yeye anavaa suti za kushonesha za mafundi wa Kitanzania na kuwataka “Watanzania kuvaa nguo, zilizobuniwa na wabunifu wa Kitanzania, na nguo za kushonesha zaidi, na kuvaa “ready made” za “made in Tanzania”.

Itapendeza mawaziri wote wa Samia, kukaa na wadau wa sekta husika kuwasikiliza, kuna vitu vizuri wadau wanavijua kuliko Serikali, hivyo kitendo cha serikali kuwasikiliza wadau, kisha kufuata ushauri, kunajenga serikali sikivu. Waziri Profesa Mkenda, naye apewe maua yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *