Hispania. Kama kuna msanii anadaiwa anapenda wanawake, basi ni Hemed PHD. Zaidi, alipenda kujinadi anapenda kujihusisha na wanawake tofauti kimahusiano na haipiti siku tatu bila kukutana na mmoja wao.
Mkali huyu wa Bongo Movie anayetamba na filamu nyingi sambamba na nyimbo za Bongo Fleva, anasema mambo hayo aliyapitia na hatamani tena kwani yalikuwa ni maisha ya kujitafuta hadi kuwa maarufu.
Akipiga stori na Mwananchi akiwa Hispania alikoshuhudia baadhi ya mechi za La Liga na kupiga picha na mastaa wa Real Madrid kama Vinicius Jr na Rodrygo mbali na ishu hiyo ya wanawake pia amefunguka jina lake jipya ni Papi Malaliga’ na kuelezea maana yake.

Kwa nini Papi Malaliga?
“Kwanza kabisa naomba niite Papi Malaliga. Hii ni kutokana na kushuhudia baadhi ya mechi huku nilipo na kuwa karibu na wachezaji maarufu wa timu mbalimbali. Sasa kwa nini nisiitwe Papi Malaliga?” anasema Hemed na kuongeza ameona watu kwenye mitandao wakikomenti vipaya kuhusu uwepo wake huko na kupiga picha na nyota hao lakini hata hivyo hajali kitu.
“Kikubwa nipo nao karibu, hao watu wa mitandaoni mimi hawanishtui kwa ‘comment’ zao na najua huo wote ni wivu wao tu. Na ukiangalia hata posti zangu mimi sijaweka caption yoyote kuhusu video au picha nilizoposti, wao nini sasa wanajielezea sana?”

Kuhusu kauli yake ya kupenda sana wanawake anasema;
“Hapana aise sio kama vile zamani, yale yalikuwa ni maisha yangu ya nyuma kwenye kujitafutia kupata umaarufu ambayo nayajutia hadi sasa. Nilikuwa natembea na wasichana hadi watano kwa siku, ilifikia hatua nikikosa mwanamke naumwa ugonjwa wa kutetemeka. Aisee yale maisha hapana na sio kitu cha kujivunia kwa sasa hivi, ila ni maisha ambayo nimeyapitia na nisingependa vijana wengi wayapitie, yana athari kubwa.”

Kwani kaacha muziki? Msikie;
“Siwezi kuacha muziki kwani kwangu ni kama burudani tu na ndiyo maana unaona nakaa muda mrefu bila kutoa nyimbo zozote. Mwanzo nilidhani utakuja kuwa ni moja ya kazi yangu, lakini imekuwa tofauti kabisa na filamu ndiyo imekuwa kama kazi yangu japo nina biashara zingine nafanya ndogondogo.”
Kwenye ngoma ni mkali;
“Na siku nikiamuaga kufanya muziki huwa nakuwa kwenye Top 5 ya wasanii wa kiume wenye kutoa nyimbo bora na hata kwenye video za nyimbo zangu huwa najua kuvaa uhusika vizuri. Hawa wasanii wenu huwa wanakimbizana wanapoona nimetia timu kwenye game ya muziki. Mimi nina kitu kikubwa sana kwenye muziki sema siufatilii kihivyo tu.”

Hiki hapa hawezi kukisahau katika sanaa
“Hiki kitu cha ‘promoter’ kuondoka na pesa yangu. Kiliniuma sana na ukizingatia nilikuwa nammudu kabisa. Yaani ilitokea nimeenda kwenye shoo Sengerema, naperform nashuka, nakuta promoter ameondoka na pesa yangu hajanilipa na tiketi ya ndege haijawa confirmed. Kwa hiyo mwishowe unaamua unachomoa fedha ambayo ipo kwenye filamu, unachukua ndege, unalipa hoteli, unatulia, Sengerema mpaka Mwanza, usafiri ni kama laki moja, kipindi hicho ukitumia gari private, sababu huwezi kupanda mabasi kwa muda huo, changamoto hii sitoisahau kabisa.”

Hemed ni mtu wa namna gani?
“Hemed ni mtu ambaye ninajipenda sana, linapokuja suala la kuvaa na kuonekana maridadi huwa natumia pesa nyingi kwani nina viatu vingi. Ukiacha raba ambazo nazo zina idadi yake na nguo ndiyo usiseme. Kutokana na wingi wa mavazi yangu nimekitenga chumba kwa ajili ya mavazi tu, humo utakuta kila aina ya nguo na viatu.”
Kitu gani unajivunia?
“Najivunia kuwa na watoto wengi na kufanana nao na nilivyo mkali kwenye suala la uzazi nina watoto zaidi ya saba na kila mtoto na mama yake.”
Ishu ya dawa za kulevya iko hivi
“Hakuna kitu kinanikwaza na kunikera zile habari za kudaiwa kutumia dawa za kulevya. Hivi kwa umri huu nashindwa kutambua athari za hizi dawa za kulevya kweli. Yaani utakuta hata nikifanya kitu tofauti huwa naambiwa nimeathirika na dawa za kulevya.”