Baada ya kuiongoza Taifa Stars kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2024, kibarua kilicho mbele ya kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Morocco ni mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco, Machi 26 mwaka huu.
Morocco anaendelea kusimamia benchi la ufundi la Taifa Stars kufuatia uamuzi wa aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Adel Amrouche kutimkia Rwanda ambako amepata fursa ya kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo ‘Amavubi’.
Hakuonekani kama Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaajiri kocha wa kigeni kwa sasa ili kushika nafasi hiyo na badala yake litaendelea na Moroco na wasaidizi wake ambao asilimia kubwa ni Watanzania na hilo linachagizwa na kauli iliyotolewa na Rais wa TFF, Wallace Karia Desemba mwaka jana akisema wana imani na Morocco.
Hii ni heshima kwa makocha wetu wazawa na mimi nazungumza siku zote na waandishi wa habari. Sijui sisi ni binadamu kunaweza kukawa na mambo mengine lakini mimi nina imani kwamba nitaendelea kuwaamini makocha wazawa na tutawapa heshima yao,” alisema Karia.
Kuaminiwa kwa Morocco kuendelea kuinoa Taifa Stars kunamfanya aingie katika orodha ya kundi kubwa la makocha wa Kiafrika ambao kwa sasa wamepewa jukumu la kuongoza timu nyingi za taifa Afrika.

Rigobert Song
Nahodha na kocha huyo wa zamani wa Cameroon kwa sasa anainoa timu ya taifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa kundi I la kuwania kufuzu Kombe la Dunia ikiwa na pointi nne.

Aliou Cisse
Baada ya kutamba akiwa kocha wa Senegal ambayo aliiongoza kutwaa ubingwa wa Afcon 2021 na mwaka uliofuata kuiongoza kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia, Aliou Cisse kwa sasa anainoa timu ya taifa ya Libya

Collin Benjamin
Nyota huyo wa zamani wa Namibia ndiye anainoa timu ya taifa ya nchi hiyo, jukumu ambalo alianza nalo tangu 2022.

Pape Thiaw
Pape Thiaw ni miongoni mwa wanasoka wenye majina makubwa Senegal na Afrika kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kikosi cha timu ya taifa ya Senegal kilichotinga robo fainali ya Kombe la Dunia 2002 akiwa mchezaji.
Kwa sasa ndiye anainoa timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kurithi mikoba ya Aliou Cisse.

Walid Regragui
Mwaka 2022, Morocco iliandika historia ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia na mafanikio hayo yalitokana na mchango mkubwa wa kocha wa nyumbani Walid Regragui.
Kocha huyo bado anaendelea kuaminiwa na taifa hilo akihudumu kama kocha mkuu.
Makocha wengine

Eric Chelle-Nigeria

Emerse Faé – Ivory Coast

Mohamed Kallon-Sierra Leone

Benni McCarthy-Kenya
Morena Ramoreboli- Botswana
Dare Nibombe- Togo
Hossam Hassan -Misri
Sami Trabelsi-Tunisia
Leslie Notsi- Lesotho
Badou Ezaki- Niger
Kwesi Appiah- Sudan
Otto Addo – Ghana
Brama Traore-Burkina Faso
Chiquinho Conde-Msumbiji
Mesay Teferi-Ethiopia
Abdourahman Okie Hadi- Djibouti
Pedro Burito- Cape Verde
Etienne Ndairagije-Burundi
Callisto Pasuwa-Malawi
Ralph Jean-Louis-Shelisheli