Mapya yaibuka dhamana ya mwigizaji Nicole

Dar es Salaam. Kufuatia kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwigizaji, Joyce Mbaga (32) maarufu Nicole Berry, na kumfanya asote rumande kwa zaidi ya siku kadhaa sasa tangu afikishwe mahakamani. Msanii mwenzake Ben Kinyaiya amesema tayari wamekamilisha masharti ya dhamana ya msanii huyo na sasa wanasubiri uamuzi wa mahakama.

Akizungumza na Mwananchi leo Machi 14,2025, Kinyaiya amesema mashabiki wake wavute subira kwani mambo ya mahakama yanaenda kisheria.

“Sisi wasanii wenzake wa Huba tumepigana kutimiza yale matakwa ya dhamana yanayotakiwa. Kwa maana ya kutafuta hati ya nyumba na hiyo pesa, bondi yenye thamani ya Sh46 milioni. Tumejitahidi kufuata sheria kwa ajili ya kumwekea dhamana ili aweze kutoka.

“Watu wasije kuona kama wasanii hatupigani tunapigana sana mwenzetu aweze kuendelea na shughuli zake na sisi tuendelee kuwa naye. Tumeshakabidhi vitu vyote vinavyotakiwa kisheria. Tunasubiri maamuzi ya mahakama ya hiyo dhamana yake,”amesema Kinyaiya.

Ikumbukwe msanii huyo na mwenzake Rehema Mahanyu (31) walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni, Jumatatu Machi 10, 2025. Wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kutokana na kupokea amana (fedha) kutoka kwa umma bila kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mbali na hayo Kinyaiya ameongezea kwa kusema kukamatwa kwa Nicole kumemuumiza na kumfanya asiwe sawa.

“Sisi ni binadamu matatizo ni ya kila mtu hakuna aliyekamilika. Mimi imeniumiza nimemzoea kwa hiyo kumkosa kidogo inanivuruga. Ni rafiki yangu wa karibu tuko wote kwenye Huba tumeigiza pamoja na mara nyingi tuko pamoja lakini sina namna,”amesema

Masharti ya dhamana

Katika masharti ya dhamana Hakimu Rugemalira, aliwataka kuwasilisha mahakamani pesa taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi cha fedha kilichotajwa kwenye shitaka, kwa mujibu wa kifungu cha 148 (5) (e), cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Kwa mujibu wa kifungu hicho, pale shitaka linapohusisha fedha zinazozidi Sh10 milioni, kupata dhamana mshtakiwa anapaswa kuwasilisha mahakamani nusu ya kiasi hicho cha fedha au mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo, kama washtakiwa ni zaidi ya mmoja basi watapaswa kuchangia kiasi sawa cha pesa.

Pia, Hakimu Rugemalira amewataka kuwa na wadhamini wawili kila mmoja, wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa na kama ni mwajiriwa awasilishe barua ya ofisi yake.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 24,2025 washtakiwa na  walirudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *