
BAO la kujifunga la kipindi cha kwanza la beki wa KMC, Abdallah Said ‘Lanso’ limeiwezesha Singida Black Stars kuungana na JKT Tanzania na Mbeya City kuwa za kwanza kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho.
Singida ilipata ushindi huo wa bao 1-0 jioni hii kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo mjini Babati mkoani Manyara.
Singida iliyoanza michuano hiyo kwa msimu huu kwa kuing’oa Magnet kwa mabao 2-0 kabla ya kuinyoosha Leo Tena kwa mabao 4-0, imeendeleza rekodi iliyonayo dhidi ya KMC katika michuno hiyo kwani msimu uliopita pia iliing’oa hatua ya robo fainali kwa kuifunga mabao 3-0.
Licha ya kuruhusu bao lililowaibulia, lakini KMC ilionyesha upinzani na kuwabana wenyeji kwa muda mrefu, ila ilipoteza nafasi za kujipatia mabao kutokana na ukuta mgumu wa Singida uliokuwa chini ya Juma Kennedy na Anthony Tra Bi Tra sambamba na kipa Obasogie.
Huo ulikuwa ni mchezo wa 10 kwa timu hizo kukutana tangu 2020, huku Singida ikiwa na rekodi ya kushinda mechi sita zikiwamo nne za Ligi Kuu na mbili za Kombe la Shirikisho, huku KMC ikishinda nne zote za Ligi Kuu na hakuna sare yoyote baina yao.
Bingwa wa michuano hiyo hukata tiketi ya ushiriki wa Kombe la Shirikisho Afrika na kwasasa watetezi ni Yanga wanaolishikilia taji kwa misimu mitatu mfululizo na ikiwa tayari imeshatinga hatua ya 16 Bora ikisubiri kuvaana na Songea United iliyopo Ligi ya Championship.
Timu zingine zilizopo hatua hiyo ya 16 Bora kuwania tiketi ya robo fainali ni Simba itakayovaana na Bigman, Tabora United itakayocheza na Kagera Sugar, huku Stand United ‘Chama la Wana’ itavaana na Girrafe Academy na Mashujaa itakwaruzana na Pamba Jiji.