
WAKATI timu zikiwa kwenye maandalizi ya Ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL), kocha wa timu ya Ukonga Queens, Denis Lipiki, amesema watawatumia wasichana kucheza ligi kwa wale waliotokea katika kituo cha Ukonga Academy.
“Tumefanya hivyo baada ya kuwaruhusu wasichana waliozidi umri, watafute timu nyingine za kuchezea,” alisema Lipiki.
Wakati akieleza hayo, alisema walianzisha kituo cha Ukonga Academy, baada ya kuona watoto wengi sana wanacheza mchezo huo katika maeneo ya Ukonga.
“Wengi wao walikuwa wametoka kuhitimu elimu ya shule ya msingi, tulipata wazo hilo na kuandaa programu maalum kwa ajili ya kuanza kuwafundisha mchezo wa kikapu kwenye Uwanja wa Chuo cha agereza (Ukonga),” alisema Lipiki.
Kwa mujibu wa Lipiki, watoto wengi waliojitokeza ni wa kike wa umri wa miaka 10 na waliwafundisha hadi wakaanza kuupenda mchezo huo.
Aliwataja wasichana waliowafundisha ni Noela Uwandameno, Hafsa Hassan, Neema na Hawa Athumani wanaochezea timu ya Vijana.
Wachezaji wengine ni Judith Nyari, Hellen Simon, Shadya Amir, Kelta Kassim na Jesca Ngisaise ( JKT Stars), Monalisa Kaijage, Witness Mapunda na Ana Marie (Jeshi Stars).
Wengine ni Winfrida Chikawe, Jacqueline Masinde, Amina Kaswa (Polisi), Gloria Manda (Donbosco Lioness) na Maria Kihivo (Pazi Queens).