
Dar es Salaam Ni sura mpya katika nafasi za ukurugenzi ndani ya Chadema, ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyojifungia kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kufanya uteuzi.
Kamati Kuu chini ya uenyekiti wa Tundu Lissu ilikutana katika kikao chake Machi 10-11, 2025, makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam, kikiwa na ajenda mbalimbali, ikiwemo uteuzi wa wakurugenzi na makatibu wa kanda.
Uteuzi huo unafanyika kujaza nafasi baada ya waliokuwa kwenye nafasi za ukurugenzi, ambao ni wajumbe wa sekretarieti, kuacha kazi.
Hatua hiyo ilijitokeza baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa uchaguzi ambapo Tundu Lissu, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bara, kushinda nafasi ya uenyekiti, akimshinda Freeman Mbowe, aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 21.
Katika uteuzi huo ulitangazwa leo Jumatano, Machi 12, 2025 na Apolinary Margwe, msaidizi katika kurugenzi ya Mawasiliano na Uenezi, hakuna mkurugenzi kati ya waliokuwepo katika nafasi hizo aliyerudishwa, huku pia kurugenzi zenyewe zikiwa zimebadilishwa.
Kurugenzi mpya kwenye utawala wa Tundu Lissu zitakuwa: Fedha na Uchumi, Sheria na Haki za Binadamu, Mafunzo na Uendeshaji, Habari, Uenezi na Mawasiliano, Chadema Digital na Ubunifu, pamoja na Diaspora na Mambo ya Nje.
Walioteuliwa kuziongoza ni Gaston Garubindi (Sheria), John Pambalu (Mafunzo na Uendeshaji), Brenda Rupia (Habari, Uenezi na Mawasiliano), Tito Kitalika (Fedha na Uchumi), John Kitoka (Diaspora na Mambo ya Nje), huku mkurugenzi wa Chadema Digital akiwa hajateuliwa.
Wakurugenzi hao wataunda sekretarieti za Chadema inayoongozwa na Katibu Mkuu, John Mnyika, na manaibu wake, Aman Golugwa (Bara) na Ali Ibrahim Juma (Zanzibar).
Miongoni mwa waliokuwepo katika kurugenzi hizo ni John Mrema (Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje) na Jonathan Mndeme (Mkurugenzi wa Sheria).
Wengine waliokuwepo ni Ludovick Lutembeka (Kurugenzi ya Fedha na Uchumi), ambapo nafasi yake aliteuliwa Tito Kitalika kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Bagamoyo, Mkoa wa Pwani hivi karibuni.
Katika kurugenzi hizo, limeanzishwa Dawati la Jinsia ambalo litakuwa linaongozwa na Catherine Ruge, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), huku Leonard Magere akiteuliwa kuwa mtaalamu wa rasilimali, miradi, na uwekezaji.
Kurugenzi za awali chini ya Mbowe zilikuwa: Fedha, Uwekezaji na Utawala, Sheria na Haki za Binadamu, Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje, Uchaguzi, na Tathmini na Ufuatiliaji.
Makatibu wa Kanda
Mbali na ajenda za uteuzi wa wakurugenzi, kikao hicho kilijadili ajenda ya uteuzi wa makatibu wa kanda za Kati, Kusini, Pwani, na Kaskazini, ambapo sura mpya pia zimeingia. Pia kilijadili taarifa ya utekelezaji wa ajenda ya ‘No reforms No Election’.
Vivyo hivyo, taarifa za ndani zinadai uteuzi wa Ruge haukuwa rahisi kupenya ndani ya kikao hicho, kutokana na majadiliano pamoja na mvutano wa wajumbe. Awali, Ruge alipendekezwa kuwa mkurugenzi wa Habari na Uenezi, lakini baadhi ya wajumbe walikataa.
Kabla ya kikao hicho, Ruge pia alipendekezwa kuwa Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi katika mkutano wa Kamati Kuu uliopita, lakini hakufanikiwa kupenya; badala yake, aliteuliwa Kitalika.
Chanzo kingine kinadai Kamati Kuu ilikuwa ya moto na mvutano kuhusu uteuzi huo, baada ya baadhi ya wajumbe kutaka waliokuwa mstari mbele katika ushindi wa Lissu kupewa nafasi hizo, lakini jambo halikuwezekana.
Mwananchi limezungumza na mmoja wa makada wa Chadema aliyechambua sura hizo mpya, akisema, “Ni uteuzi halali kwa sababu umefanywa na mamlaka halali kabisa, lakini ni uteuzi ambao haujakidhi matarajio ya wengi hasa katika baadhi ya nafasi.”
Mwanachama huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake, aliyewahi kuwa mgombea ubunge mwaka 2020, amesema: “Katika huu uteuzi, mfano mmoja kati ya sera kubwa iliyompa umaarufu Lissu ni kufanya mabadiliko makubwa ya sekretarieti ya kuweka watu wanaokwenda na wakati. Hivyo, uteuzi huu ulisubiriwa sana na watu.
“Sasa, kwa mujibu wa uzoefu wangu, walioteuliwa ni watu ambao hawana uzoefu wa kutosha hasa kwenye siasa za ushindani, ukimwacha Pambalu ambaye kitaaluma ni mwalimu, amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Bavicha.”
Ameendelea kusema: “Msemaji anapaswa kujua chama kwa kiwango cha juu zaidi, historia, sera, itifaki kwa sababu mara kwa mara atazungumza kwa niaba ya chama, unahitaji mtu anayeijua na sisemi kwamba hafai, lakini nafasi aliyopewa ni kubwa kuliko uwezo wake.”
Mjumbe huyo wa zamani wa Baraza Kuu amesema: “Taasisi kama ya Chadema ilipofikia, nafasi zinazoteuliwa inapaswa kuwa watu wanaojulikana hasa kabla ya kuteuliwa. Yaani tulipofikia, ukimteua mtu hawaulizani ‘huyu ni nani?’ Lakini sasa unamteua mtu na wanaanza kuulizana ‘huyu ni nani?’ Hii inatia shaka. Lakini wacha tuwape muda, wanaweza kuja na mawazo mapya.”
Walioteuliwa kina nani?
Pambalu amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) kuanzia mwaka 2019/20. Pia amewahi kuwani ubunge wa Nyamagana, mkoani Mwanza, lakini hakufanikiwa. Aligombea uenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, lakini hakufanikiwa mbele ya Ezekia Wenje.
Amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2024. Alijitosa kutetea nafasi yake, lakini hakufanikiwa mbele ya wakili mwenzake, Dickson Matata.
Ni mbunge wa zamani wa viti maalumu kuanzia mwaka 2015/20. Amewahi kuwani ubunge jimbo la Serengeti, lakini hakufanikiwa. Amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), alijitosa tena kutetea nafasi hiyo, lakini hakufanikiwa mbele ya Pamela Massay.
Huyu sio maarufu ndani ya Chadema, lakini ni Katibu wa Bawacha Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Makatibu wa kanda wateuliwa
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Kamati Kuu walifanya uteuzi wa makatibu wa kanda nne za Kati, Kaskazini, Kusini, na Pwani.
Walioteuliwa ni: Totinan Ndonde (Kanda ya Kaskazini), aliyewahi kuwa ofisa wa Kanda Kaskazini, na Ashura Masoud (Kanda ya Kati), aliyewahi kugombea uenezi wa Bawacha katika uchaguzi uliofanyika Januari 2025.
Ashura anachukua nafasi ya Emmanuel Masonga, huku Ntele Benjamin (Kanda ya Pwani) akichukua nafasi ya Jerry Kerenge aliyekuwa akikaimu wadhifa huo.