Mmoja Morogoro asombwa na maji, akutwa kwenye karavati

Morogoro. Mwanaume mmoja ambaye hajafahamika jina, mkazi wa kata ya Mkundi, mkoani Morogoro amenusurika kufa baada ya kusombwa na maji kufuatia mvua iliyonyesha kuanzia jana jioni hadi leo Jumatano, Machi 12, 2025 alfajiri.

Mvua hizo ambazo zinanyesha maeneo mbalimbali nchini kama zilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambapo zilitoa tahadhari za kuchukuliwa kufuatiwa uwezekano wa kuwapo mvua nyingi.

Akizungumza na Mwananchi asubuhi ya leo Jumatano, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo amesema mwanamume huyo  alisombwa na maji jana usiku huko Mkundi na aliokolewa baada ya kunasa kwenye karavati.

“Mwanaume huyu alikuwa akivuka mahali ambapo maji yanapita hivyo aliteleza na kusombwa na maji baada ya kupata taarifa tulifuatilia uelekeo wa maji na tukafanikiwa kumwokoa akiwa amenasa kwenye karavati.”

“Baada ya kuokolewa, mwanamume huyo hakupata madhara makubwa zaidi ya kuchoka kutokana na kupigwa na maji, baadaye ndugu zake walikuja na kumchukua,” amesema.

Akizungumzia maeneo mengine ya mkoa wa Morogoro, Kamanda Marugujo amesema mpaka sasa hakuna taarifa ya madhara yoyote katika wilaya nyingine, japokuwa baadhi ya maeneo mvua zimeanza kunyesha.

“Mvua ndio zimeanza kunyesha na tunaendelea kufuatilia huko wilayani kupitia kwa makamanda wa wilaya, hii mvua ya kwanza inaweza isiwe na madhara kutokana na jua kali lililowaka siku za nyuma, isipokuwa mvua hii iliyonyesha usiku ikirudia tena leo upo uwezekano wa kutokea madhara,” amesema Marugujo.

Kwa mujibu wa utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa itakayopata mvua nyingi.

Hivyo Kamanda Marugujo amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa watoto wanaoishi kwenye maeneo hatarishi ikiwamo mabondeni, jirani na mito, makorongo na mabwawa.

Aidha amewaelekeza wananchi kupiga simu ya 114 endapo wataona majanga yatakayotokana na mvua hizo, lakini pia kutokaa chini ya miti na pembeni mwa kuta za nyumba Kwa kuwa mvua hizo zimekuwa zikiambatana na upepo mkali.

Mmoja wa wananchi wa kata ya Lukobe ambayo ni moja ya maeneo yaliyopata mvua usiku kucha, Joseph Mgabo amesema mvua hizo zilianza saa 12 jioni zikiambatana na mvua ya mawe na baadaye ilinyesha ya kawaida.

“Mimi nikiwa kwenye shughuli zangu za biashara ghafla ulikuja upepo mkali ulioambatana na radi na baadaye ilianza kunyesha hata hivyo nilianza kusikia kwenye bati vitu vinadondoka mithili ya mawe madogo, nilipotoka nje ndio nikaona vipande vya barafu vikitoka angani na kudondoka chini,” amesema Mgabo.

Amesema mvua hiyo ya mawe haikuchukua muda mrefu ilikata na baadaye ikaanza kunyesha ya kawaida.

Jana Jumanne Machi 11,2024, TMA iliyotoa utabiri wa hali ya hewa ikitoa angalizo la mvua kubwa katika maeneo machache ya Pwani ya Kusini mikoa ya Lindi na Mtwara, Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa, Songwe na Njombe.

Aidha ilieleza mikoa ya Ruvuma, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro iliyotarajiwa kunyesha mvua jana na maeneo mengi mvua zimenyesha. 

Taarifa hiyo ya TMA inaonyesha leo mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Lindi na Mtwara kuwapo uwezekano wa mvua kunyesha huku wananchi wakitakiwa kuchukua tahadhari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *