Dar es Salaam. Maria Sarungi na watoto wengine wawili wa Profesa Philemon Sarungi wameomboleza msiba wa baba yao wakiwa ughaibuni, baada ya kushindwa kuhudhuria mazishi yake nchini Tanzania.
Watoto hao wameomboleza msiba huo kwa kutumia sauti zilizochezwa wakati wa hafla ya kutoa heshima za mwisho kwa Profesa Sarungi iliyofanyika katika viwanja wa Karimjee, jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu, Machi 10, 2025.
Tofauti na Maria aliyesema ameshindwa kuhudhuria kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake kiusalama, watoto wengine, Martin na Emok, hawakueleza sababu.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakiwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga mwili wa Profesa Philemon Sarungi. Picha na Sunday George
Profesa Sarungi alifariki dunia Machi 5, 2025 kwa maradhi ya moyo na atazikwa leo, Machi 10, katika makaburi ya Kinondoni.
Akimzungumzia baba yake kupitia sauti iliyochezwa studio, Maria Sarungi amesema mzazi wao huyo amewahi kuwaambia maisha ni mapambano na bila kufanya hivyo hutafanikiwa.
Amesema hilo amelisisitiza hata kwenye kitabu chake chenye jina la Maisha ni Mapambano, kilichojenga msingi, usawa kwa wote, ujasiri na utu.
“Alitwambia mtu wa hali ya chini na juu wote ni sawa,” amesema.
Maria, anayeishi Nairobi nchini Kenya, amesema pamoja na watu wengine kumfahamu kuwa mwanasiasa na katika nafasi mbalimbali, wao walibahatika kumjua kwa kuwa ni baba yao na mwalimu wa maisha yao.
Amesema wameshuhudia akiendelea kukutana na watu hata baada ya kustaafu, akiendelea kukutana na watu na hakuacha kujaribu kumsaidia yeyote aliyemuomba msaada.

Waombolezaji wakiwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga mwili wa Profesa Philemon Sarungi. Picha na Sunday George
“Hakuwahi kuwa tajiri wa mali lakini alikuwa tajiri wa watu na mahusiano, na uwepo wenu hapa ni ushuhuda wa utajiri wake wa upendo na heshima aliyojijengea katika jamii,” amesema.
Amesema amewajengea pia uaminifu, imani, na hofu ya Mungu, na zaidi aliipenda Tanzania na kuwajenga katika msingi wa kutumikia nchi sio kwa kujinufaisha.
“Ingawa sitaweza kuja kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu kiusalama, nina imani kuwa ipo siku tunaonana akhera baba,” amesema.
Kwa upande wa sauti ya mtoto wake wa kwanza, Dk Emok Sarungi, ameshukuru kwa maisha ya baba yake, huku akisimulia walivyokutana siku za karibuni.
Amesema anaamini ataendelea kuwepo katika maisha yao hasa kwa kuwa kuna wajukuu wake bado wanaishi.
“Nakupenda na nitakukumbuka, tunakupenda na tutakukumbuka, Mungu akuweke mahala pema peponi,” amesema.
Ujumbe kama huo umetolewa pia na Martin Sarungi, mtoto mwingine wa Profesa Philemon Sarungi.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu (kushoto) akisalimiana na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana walipokutana leo Jumatatu Machi 10, 2025 katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kumuaga Profesa Philemon Sarungi.
Amesema atamkumbuka baba yake kwa malezi bora na ataendelea kuenzi mafunzo yake.
Mbali na salamu za watoto hao, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amesema kiongozi huyo amepigana vita vyake vizuri na ameilinda nchi yake.
“Mimi ambaye sijawahi kuwa mwanafunzi wake wa mifupa, nafahamu mengi kuhusu mifupa, hivyo nafahamu kazi yake kwa sababu na mimi nina ufahamu kidogo na masuala ya mifupa.
“Tuko hapa kusheherekea maisha ya Mtanzania huyu wa kipekee kabisa. Uwepo wake unaonyesha bado tunaweza kutengeneza nchi bora zaidi,” amesema Lissu.
Amesema jana alikutana na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, na alimwambia alikuwa akibishana sana na Profesa Sarungi kuhusu Simba na Yanga.