Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania na Klabu ya Al Talaba inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq maarufu kama ‘Iraq Stars League’, Simon Msuva ameifungia mabao mawili timu yake katika mchezo wa Ligi dhidi ya Naft Al Junoob.
Katika mchezo huo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Fayhaa ilishuhudiwa Msuva akifunga bao la kwanza katika dakika ya 25 ambapo alimalizia krosi iliyopigwa kichwa na Louai al-ani.
Katika dakika ya za majeruhi, Msuva alifunga kwa mara ya pili akiiandikia timu yake bao la pili na kuihakikishia kupata pointi tatu muhimu kwani mpaka dakika 90 zinamalizika Al Talaba ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0.

Mabao mawili aliyofunga jana dhidi ya Naft Al Junoob yanamfanya Msuva kufikisha idadi ya mabao sita kwenye Ligi Kuu ya Iraq ikiwa ni msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu.
Baada ya ushindi huo Al Talaba imesogea mpaka nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 37 katika mechi 22 ilizocheza huku ikizidiwa pointi tisa na vinara wa Ligi hiyo Zakho yenye pointi 46.

Naft Al Junoob yenyewe imesalia katika nafasi ya 17 ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 22 huku ikifungwa mechi 12, sare mechi nne na kupata ushindi mechi sita.
Al Talaba itashuka tena dimbani Machi 14, 2025 ambapo itakuwa kwenye Uwanja wa nyumbani kuikabili Newroz inayoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Iraq ambao una jumla ya timu 20.