
Unguja. Wakati Serikali ikihamasisha uvuvi salama na endelevu, baadhi ya wavuvi wametaja changamoto kubwa inayochangia uvuvi haramu na kuharibu matumbawe (mazalia ya samaki) kuwa ni ukosefu wa zana na vifaa vya kisasa.
Hayo yamebainishwa na wajumbe wa kamati za uvuvi kutoka Kijiji cha Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja, leo Jumatatu, Machi 10, 2025, wakati wakijengewa uwezo kuhusu uvuvi salama, unaolinda bahari na kuhifadhi rasilimali zake.
“Tupo tayari kutunza mazingira na kuendesha uvuvi salama, lakini tunaomba kuangaliwa kwenye zana. Tupewe vifaa vya kisasa kwani uvuvi huu tunaotumia wa kutumia tanga na mti unachangia kuharibu matumbawe,” amesema Ali Bai.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mjumbe wa Kamati ya Uongozi, Mcha Khamis, aliyesema iwapo watapatiwa vifaa vya kisasa, changamoto za uvuvi zitapungua kwa kiasi kikubwa.
Hivyo, wameiomba Serikali kuwawezesha kwa kuwapatia vyombo vya kisasa, kwani uvuvi wa kutumia tanga na mti kwa upepo unaathiri matumbawe yaliyo chini ya bahari.
Ofisa Msimamizi Shirikishi, Maryam Ramadhan Mwinyi, kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, amesema kamati za uvuvi zina jukumu kubwa la kusimamia ulinzi shirikishi ili kupambana na uvuvi haramu usiendelee kufanyika katika maeneo ya hifadhi na kuimarisha rasilimali zilizopo.
“Kamati hazitakiwi kushiriki uvuvi haramu ili kuzifanya rasilimali za bahari kuwa endelevu,” amesema Maryam.
Amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuwa na utaratibu wa kutunza kumbukumbu ya vifaa pamoja na matumizi ya fedha za kamati ili kuondoa migogoro inayotokana na matumizi mabaya ya fedha za kamati.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Hifadhi ya Bahari (Tumca), Mwanajuma Ali, amesema kamati za shehia zina wajibu mkubwa wa kusimamia rasilimali za bahari kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye Ofisa Uhifadhi wa Mazingira, Bioanuai na Rasilimali za Bahari, Thuwaiba Kassim Haji, kutoka Idara ya Uhifadhi wa Bahari, amesema Serikali kupitia idara hiyo imeweka utaratibu wa kufanya uchaguzi wa kamati za uvuvi kwa lengo la kutunza mazingira ya bahari pamoja na rasilimali zake.
Amesema kuwepo kwa kamati za uvuvi kunasaidia kudhibiti uvuvi haramu na uharibifu wa matumbawe, ambao unaathiri mazalia ya samaki baharini.
Kwa upande wake, Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Haji Nahoda, amezitaka kamati za uvuvi Zanzibar kusimamia wavuvi wakati wa ukataji wa leseni kwa kufuata taratibu zilizowekwa ili kutambua aina ya uvuvi na zana zitakazotumika baharini, hivyo kuondokana na matumizi mabaya ya rasilimali za bahari.