TFF yavifungia tena viwanja vitatu

Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kufungia viwanja vitatu kutumika kwa michezo ya ligi kutokana na kukosa vigezo vya kikanuni na kisheria vinavyotakiwa kutumika kwa Ligi Kuu.

Viwanja vilivyokumbana na rungu hilo ni Jamhuri (Dodoma), CCM Kirumba (Mwanza) na Liti (Singida). 

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Machi 10, 2025, na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo imesema miundombinu ya viwanja hivyo haikidhi masharti yaliyowekwa katika Kanuni ya Leseni za Klabu.

Hivyo, timu zinazotumia viwanja hivyo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia viwanja vingine vinavyokidhi vigezo hadi marekebisho yatakapofanywa na TFF kufanya ukaguzi upya. 

“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limevifungia viwanja vya Jamhuri Dodoma, CCM Kirumba Mwanza na Liti Singida kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

“Miundombinu ya viwanja hivyo haikidhi matakwa ya Kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu.

“Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia viwanja hivyo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia viwanja vingine kama Kanuni inavyoelekeza mpaka viwanja hivyo vitakapofunguliwa, baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF.

“TFF inazikumbusha Klabu zote kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja,” imefafanua taarifa hiyo.

TFF imezikumbusha klabu zote kuendelea kuboresha miundombinu ya viwanja ili kuhakikisha michezo inachezwa katika mazingira salama na yanayokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Uamuzi wa kufungia viwanja hivyo umetolewa siku chache baada ya TFF kuufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kutokana na kuwa na eneo lisiloridhisha la kuchezea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *