Arsenal yapata mrithi wa Edu

London, England. Baada ya mchakato wa  muda mrefu, Arsenal wanadaiwa kufikia makubaliano ya kumuajiri mkurugenzi wa zamani wa michezo wa Atletico Madrid, Andrea Berta, kuwa mrithi wa Edu katika nafasi hiyo hiyo.

Berta aliondoka Atletico baada ya miaka 12, Januari mwaka huu na amekua katika mazungumzo na viongozi wa juu wa Arsenal tangu wakati huo ambao wamevutiwa na kazi nzuri aliyoifanya akiwa  Hispania ambapo aliifanya Atletico kuwa timu shindani mbele ya Real Madrid na Barcelona licha ya ukubwa wa timu hizo.

Mbali ya Atletico,  Berta pia amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa michezo wa timu nyingine kama Parma na Genoa za Italia.

Berta aliisaidia Atletico kupata mafanikio makubwa kuanzia ligi ya ndani na michuano ya kimataifa ambapo katika kipindi chake timu hiyo ilishinda mataji mawili ya  La Liga, Europa League na kumaliza kama washindi wa pili wa Ligi ya Mabingwa mara mbili.

Vilevile aliwanunua na kuwauza Antoine Griezmann na Rodri kwa kiasi kikubwa cha fedha na msimu uliopita alitumia pauni milioni 180  kuwanunua Julian Alvarez, Conor Gallagher, Robin Le Normand na Alexander Sorloth ili kuimarisha tena kikosi cha Diego Simeone.

Edu aliondoka katika viunga vya Emirates Novemba mwaka jana akidaiwa kwenda kuchukua nafasi ya  Mkurugenzi wa timu zinazomilikiwa na tajiri Evangelos Marinakis.

Kundi hilo linajumuisha timu ya Nottingham Forest ambayo imekuwa kivutio kwenye Ligi Kuu England msimu huu.