FCC yawasisitiza wafanyabiashara kulinda haki za mlaji

Dar es Salaam. Wakati Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji yakitarajiwa kufanyika Machi 17 mwaka huu, wafanyabiashara na watoa huduma  nchini wamehimizwa kuzingatia haki za mlaji wanaposambaza bidhaa na huduma sokoni.

Wito huo umetolewa leo Machi 7, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), William Erio katika hafla fupi ya maadhimisho wiki ya kumlinda mlaji ambayo kwa mwaka huu kilele chake kinatarajiwa kuwa Machi 17,2025.

Erio amesema mlaji ana haki nane na baadhi ya haki hizo ni usalama wa bidhaa na huduma anazopata, haki ya kupata taarifa kuhusu bei, ujazo na malighafi zilizotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali.

“Haki hizo zinatambulika kimataifa tangu zilipoundwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) mwaka 1980″amesema.

Pia amesema kuwa pamoja na kuwa na haki mlaji ana wajibu ambao anapaswa kuzingatia anaponunua bidhaa ikiwemo kuwa makini na kusoma maelekezo ya bidhaa.

“Mtumiaji wa bidhaa ana wajibu wa kuuliza taarifa zote muhimu kuhusu bidhaa au huduma anayokwenda kuitumia ili kufahamu ubora na matumizi yake sahihi,” amesema.

Anasema kuzingatiwa kwa haki hizo ni muhimu kwani kutamfanya mtumiaji wa bidhaa au huduma kuwa salama.

Ameongeza kuwa kutokana na baadhi ya watu kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na haki hizo kuelekea kilele cha maadhimisho hayo wataendelea kutoa elimu kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kliniki za walaji pamoja na kutoa semina kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na makundi mengine katika jamii.

Pia kupitia maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Haki za Mlaji yatakayofanyika Machi 17,2025 jijini  Dar es Salaam ambayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo.

“Maadhimisho haya yanatoa fursa kwa FCC kama Mamlaka ya Kusimamia Masuala ya Kumlinda Mlaji kwa kutimiza wajibu wake kisheria wa kutoa elimu kwa umma kuhusiana na haki, wajibu na nafuu zilizopo na kuwakumbusha wadau wote ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara, kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na kuheshimu misingi ya ushindani,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa udhibiti wa mienendo ya biashara zisizofaa,  Magreth Otouh amesema mlaji akijua haki na wajibu wake ipasavyo itasaidia hata katika kudhibiti uuzwaji wa bidhaa zisizokidhi ubora.

FCC ilianza maadhimisho hayo Machi 8, 2024 katika ofisi zake kwa kutoa elimu kupitia redio na mitandao ya kijamii na semina kwa wadau katika sekta mbalimbali.