
Ikiwa ni miaka minne tangu kiwanda cha muziki wa Bongo Fleva kumpokea msanii Platform na kumthibisha kama moja ya bidhaa bora kwenye soko la muziki.
Msanii huyo ameiamba Mwananchi Scoop, migogoro kati yake na uongozi wake ilipelekea ayumbe kimuziki mwaka 2024
” Kiukweli nisiwe muongo mwaka jana sikuweza kufanya vizuri kabisa. Lakini namshukuru Mungu mapokezi ya mwaka huu yanaridhisha, na mapokezi ni makubwa.
“Ukiangalia wimbo wangu wa ‘Yako Wapi’, lakini nikaja kutoa back to back hapa nikatoa Why na mapokezi yamekuwa makubwa hata ukiangalia komenti za wadau,” amesema Platform.
Hata hivyo, msanii huyo amesema kwa sasa amemaliza mgogoro kati yake na uongozi. Amesema licha ya changamoto hizo hakuweza kubadilisha uongozi kwa sababu mkataba wake ulikuwa bado haujaisha.
“Menejimenti ni ileile kwa sababu mimi na wao mkataba unaisha mwaka huu, kwa hiyo ilikuwa inanilazimu nisikilize mkataba uishe. Alafu niangalie kama nitasaini tena ama niondoke,” amesema Patform.
Mbali na hayo, msanii huyo amefichua kuwa kutokana na kufanya vibaya 2024, alipitia wakati hadi kujihisi ana tatizo la afya ya akili.
“Kuanzia 2023 mwishoni mpaka 2024, mwaka mzima nilikuwa napitia wakati mgumu, kiukweli kama sio mwanaume unaweza kujikuta pia unaingia kwenye vitu vya hatari kama madawa au ulevi.
“Nashukuru Mungu watu ambao nipo nao, familia yangu, na watu ambao walikuwa karibu na mimi walihakikisha kila kitu kinakuwa sawa na kurudi kwenye gemu. Kwa hiyo mimi pia ni mhanga wa hayo majanga naweza nikasema hivyo,” amesema Platform.
Sambamba na hayo msanii huyo aliwahi kuapa kwamba hatafanya kazi na wasanii wa kike lakini kupitia Mwananchi Scoop ametengua kauli yake.
“Hilo limepita kwa sababu unajua sisi wanadamu mara zote hatujakamilika, muda mwingine mtu unakuwa na hasira. Nilikuja kugundua kuwa sikupaswa kufanya hivyo kwasababu mtu anapokosea anapaswa kuelekezwa.
“Ukizingatia wanawake wana mchango mkubwa sana katika jamii, lakini pia hata katika maisha,”amesema
Platform kwa sasa anatamba na kazi yake mpya inayoenda kama Why ikiwa na siku 12 tangu kutoka kwake.
Pia ameahidi kuachia album yake ya kwanza ambayo itakuwa kazi kubwa baada ya Ep yake ya Above And Beyond iliyotoka mwaka 2023.