
WANASEMA mchezo wa Dabi hauna mwenyewe. Mara kadhaa matokeo yake huwa ya kushangaza yakiwa hayajatarajiwa na wengi, lakini wakati mwingine wazoefu wana nafasi yao kubwa ya kufanya vizuri.
Jumamosi hii kwenye Uwanja Benjamin Mkapa,Dar es Salaam, Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba katika Kariakoo Dabi ya 114 kwenye Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo umebeba hisia nyingi huku ukiwakutanisha makocha wakuu wa timu hizo kwa mara ya kwanza licha ya kwamba Fadlu Davids wa Simba kwake itakuwa ni Kariakoo Dabi ya tatu.
Miloud Hamdi wa Yanga aliyetambulishwa kikosini hapo Februari 4, 2025, anakwenda kukaa benchi kuiongoza Yanga katika mchezo wake wa sita baada ya mitano nyuma kushinda minne na sare moja.
Makocha hao wanapokwenda kukutana kwa mara ya kwanza, rekodi zinaonyesha kila mmoja amewahi kucheza mechi ya dabi katika maisha yake ya kufundisha.
Fadlu aliyetokea Raja Casablanca ya Morocco akiwa kocha msaidizi na kukabidhiwa ukocha mkuu Simba Julai 5, 2025, ana uzoefu wa kucheza dabi nne tangu atue Tanzania.
Katika dabi hizo nne, amefanikiwa kushinda moja pekee dhidi ya Azam ikiwa ni Mzizima Dabi kwa mabao 2-0 ukiwa ni mchezo wa duru la kwanza la Ligi Kuu Bara uliochezwa Septemba 26, 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Tayari Fadlu amepoteza dabi mbili na zote dhidi ya Yanga akianza Ngao ya Jamii Agosti 8, 2024 akifungwa 1-0, kisha Ligi Kuu Bara duru la kwanza Oktoba 19, 2024 akipoteza kwa bao 1-0.
Lakini ana sare moja ya Mzizima Dabi aliyoipata Februari 24, 2025 ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara duru la pili.
Kwa upande mwingine, Fadlu wakati yupo Afrika Kusini, alikuwa kocha wa muda kuiongoza Orlando Pirates iliyocheza Dabi ya Soweto mbili dhidi ya Kaizer Chiefs na kupoteza zote.
Wakati huo Orlando Pirates ilikuwa na makocha wawili wa muda, Fadlu na Mandla Ncikazi walioshika kijiti kilichoachwa na Josef Zinnbauer.
Hiyo ilikuwa msimu wa 2021-2022 ambapo matokeo yalikuwa hivi; Mamelodi Sundowns 4-1 Orlando Pirates na Orlando Pirates 0-2 Mamelodi Sundowns.
Katika rekodi za dabi, hii tunaweza kuiweka pembeni kwani Fadlu hakusimama peke yake kwani alishirikiana na Ncikazi lakini bado inabaki kuwa sehemu ya kuzicheza dabi.
Pale Morocco akiwa kocha msaidizi wa Raja Casablanca, amekuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo katika dabi yao dhidi ya Wydad ambazo zote mbili chama lake lilishinda katika msimu wa 2023-2024.
Kwa upande wa Hamdi, amezicheza dabi nne akiwa Algeria wakati anaifundisha USM Alger kwa vipindi viwili tofauti.
Kocha huyo mwenye uraia wa Algeria na Ufaransa, katika dabi hizo nne maarufu kwa jina la Dabi ya Algiers ambayo huzikutanisha USM Alger na MC Alger, ameshinda moja na sare tatu, hajapoteza huku ikishuhudiwa msimu wa 2015-2016 akibeba pia ubingwa wa Ligi Kuu Algeria.
Katika kipindi chake cha kwanza akiwa kocha wa USM Alger ambapo alibeba ubingwa wa ligi, alianza kuifundisha timu hiyo kuanzia Julai 1, 2015 hadi Juni 30, 2016 akikutana mara mbili na watani zake wa jadi, MC Alger.
Katika msimu huo, mechi zote hazikuwa na mshindi matokeo yakiwa 0-0 na 2-2.
Baada ya kuondoka na kurejea kuifundisha tena USM Alger kuanzia Novemba 12, 2017 hadi Juni 30, 2018, ndipo alipopata ladha ya ushindi wa dabi akiichapa MC Alger mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Novemba 28, 2017 ugenini kisha nyumbani matokeo yakawa 2-2.
Ukiangalia takwimu za dabi ambazo makocha hao wameziongoza timu zao, Hamdi amekuwa na matokeo mazuri kidogo akiwa bado hajapoteza kati ya nne wakati Fadlu akipoteza mbili tena zote dhidi ya Yanga ambayo anakwenda kukabiliana nayo ikiwa chini ya Kocha Hamdi.
Wakati Fadlu anapoteza dabi zote mbili msimu huu mbele ya Yanga, alikutana na Miguel Gamondi, huku Mzizima Dabi mbili ilikuwa dhidi ya Rachid Taoussi.