
HII inaweza kuwa taarifa njema kwa mashabiki wa Yanga, baada ya kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephane Aziz KI kuonekana hospitalini akiwa na mkewe, Hamisa Mobetto, staa huyo ameingia kambini juzi na kufanya kikao cha siri na kocha Miloud Hamdi.
Taarifa hiyo iliwashtua mashabiki wengi wa Yanga, kwani Aziz KI ni miongoni mwa mastaa tegemeo wenye uwezo wa kuamua mechi kubwa.
Katika misimu mitatu aliyochezea Yanga, unaweza kusema ana uzoefu na dabi kwani amewahi kuifunga Simba mabao matatu na asisti moja katika michezo saba ya ligi waliyokutana.
ATINGA MAZOEZINI
Aziz KI juzi alitinga mazoezini, akionekana kutembea vizuri, hiyo ikimaanisha kuwa hali ya kiungo huyo imeanza kutengamaa.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa, kiungo huyo alifika kambini siku ya juzi lakini hakufanya mazoezi yoyote.
“Aliingia kambini jana (juzi) jioni na alipofika alionekana anatembea vizuri kidogo, lakini kwa sisi tunaomfahamu ni wazi kuwa ule sio mwondoko wake.
“Licha ya kutokuonekana mazoezini, alikutana na kocha na kufanya naye kikao cha siri, lakini haijulikani walizungumza nini.”
ILIVYOKUWA
Hapo awali, Mwanaspoti iliandika kuwa, kiungo huyo baada ya kurudi mjini na kikosi cha Yanga alionekana kuwa na maumivu ya mgongo, hali iliyomfanya ashindwe kutembea vizuri.
Halafu siku mbili baadaye, alionekana katika hospitali ya Saifee, iliyoko jijini Dar es Salaam, akiwa ameshikwa mkono wa kulia na mkewe.
Huku kwa mwonekano, Aziz Ki alikuwa akichechemea na kutembea taratibu mithili ya mtu anayepata maumivu katika nyonga zake, hivyo mkewe alitumia dakika mbili kutoka naye ndani mpaka kuingia katika gari aina ya Range Rover lililokuwa limeegeshwa nje ya hospitali hiyo.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa, Aziz Ki alikuwa akionekana hospitalini hapo kwa siku tatu mfululizo akifika na kuelekea katika eneo la tiba mazoezi (fiziotherapia).
Mastaa wa Yanga wako kambini tangu Jumamosi kujinoa kwa ajili ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba itakayochezwa keshokutwa Jumamosi kuanzia saa 1:15 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa.