China yajibu vita ya kibiashara dhidi ya Trump

Beijing. Baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuanzisha utekelezaji wa amri ya kupandisha ushuru kwa bidhaa kutoka China, nchi hiyo imejibu kwa hatua za kisasi.

Taarifa iliyochapishwa na Ubalozi wa China nchini Marekani kwenye ukurasa wa X, ilidai kuwa, kile kinachofanywa na Marekani ni matokeo ya hasira zao kutokana na kuingizwa nchini humo kwa dawa za kutuliza maumivu makali aina ya Fentanyl zinazotoka China.

Marekani ilikosoa magenge ya dawa za kulevya kutoka Mexico kwa kusambaza Fentanyl, mwaka 2022 dawa hiyo ilisababisha vifo 109,680 nchini Marekani.

Katika taarifa hiyo, Ubalozi wa China ulisisitiza kuwa,  Marekani inapaswa kufanya mashauriano ya usawa na China ili kutatua suala hilo.

“Ikiwa Marekani inataka kweli kutatua tatizo la Fentanyl, jambo sahihi ni kushauriana na China kwa kuheshimiana kama wenza sawa. Ikiwa Marekani inataka vita iwe ni vita vya ushuru, vita vya kibiashara au aina nyingine yoyote, tuko tayari kupambana hadi mwisho,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilikataa malalamiko ya Marekani kuhusu Fentanyl kama sababu halali ya kuongeza ushuru kwa bidhaa za China.

Msemaji wa wizara hiyo alisisitiza kuwa hatua za China za kulinda haki na masilahi yake ni halali na muhimu.

 “Badala ya kutambua juhudi zetu, Marekani imejaribu kutuchafua na kutulaumu, huku ikitumia ongezeko la ushuru kama shinikizo na uonevu dhidi ya China. Wanatuadhibu kwa kuwasaidia. Hili halitatatua tatizo la Marekani na litahujumu mazungumzo na ushirikiano wetu wa kupambana na dawa za kulevya,” inasema taarifa hiyo.

                 

Ushuru mpya wa Marekani

Utawala wa Trump umeweka ushuru wa ziada wa asilimia 10 kwa bidhaa za China, baada ya ushuru wa asilimia 10 uliokuwa tayari unatumika.

Ushuru huu mpya ulianza kutekelezwa Jumanne. ushuru kama huo pia umewekwa kwa bidhaa kutoka Canada na Mexico zinazoingia Marekani kwa sababu hiyo hiyo.

Kauli kutoka kwa msemaji wa China ilitolewa baada ya Serikali ya Trump kuongeza ushuru kwa bidhaa zote za China hadi asilimia 20 kutoka asilimia 10, kulingana na ripoti ya CNN.

China ilijibu Jumanne kwa kutangaza ushuru wa asilimia 15 kwa uagizaji wa kuku, ngano, mahindi na pamba kutoka Marekani, kulingana na taarifa kutoka Tume ya Ushuru ya Baraza la Serikali.

Aidha, ushuru wa asilimia 10 uliongezwa kwa “sorghum, soya, nyama ya nguruwe, nyama ya ng’ombe, bidhaa za samaki, matunda, mboga na bidhaa za maziwa,” inasema taarifa hiyo.

Wizara ya Biashara ya China pia iliongeza kampuni 15 za Marekani, ikiwa ni pamoja na mtengenezaji wa droni Skydio, kwenye orodha yake ya udhibiti wa usafirishaji nje, hatua inayozuia kampuni za Kichina kuuza vifaa vyenye matumizi ya kijeshi kwa kampuni hizo, kulingana na CNN.

Ushuru wa kisasi wa China ulilenga sekta zinazohusiana zaidi na wafuasi wa utawala wa Trump, alisema Alfredo Montufar-Helu, mkuu wa Kituo cha China cha Conference Board.

Alibainisha kuwa ushuru wa China unatoa nafasi kwa mazungumzo ili kuepuka ushuru wenye madhara makubwa zaidi baadaye.

Vita vya kibiashara vya Trump

Rais Donald Trump alianzisha vita vya kibiashara dhidi ya washirika wakuu watatu wa biashara wa Marekani, jambo lililosababisha hatua za kisasi kutoka Mexico, Canada na China, huku masoko ya kifedha yakitikiswa kutokana na hofu ya mfumuko wa bei na hali ya kutokuwa na uhakika kwa biashara.

Muda mfupi baada ya Trump kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zinazotoka Mexico na Canada, aliweka ushuru wa asilimia 10 tu kwa nishati kutoka Canada.

Aidha, aliongeza ushuru kwa bidhaa za China kutoka asilimia 10 hadi asilimia 20.

Beijing ilijibu kwa kuweka ushuru wa hadi asilimia 15 kwa bidhaa mbalimbali za kilimo kutoka Marekani.

Pia, ilipanua orodha ya kampuni za Marekani zinazokabiliwa na udhibiti wa mauzo ya nje na vizuizi vingine kwa kuongeza takriban kampuni 24 zaidi.

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, alisema nchi yake itaweka ushuru kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 100 ndani ya siku 21.

“Leo, Marekani imeanzisha vita vya kibiashara dhidi ya Canada, mshirika wao wa karibu zaidi, rafiki yao wa karibu zaidi.

“Wakati huo huo, wanazungumzia kushirikiana na Urusi na kumpendelea Vladimir Putin, dikteta muongo na mwenye damu mikononi mwake. Hii ina maana gani?” alisema Trudeau.