
Unguja. Siku chache baada ya kuzinduliwa stendi kuu ya kisasa Kijangwani na kulazimisha daladala kupitia kwenye kituo hicho, wananchi na abiria wamelalamikia mzunguko mkubwa unajitokeza na kusababisha kero.
Stendi hiyo ya kisasa ilizinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Januari mwaka huu katika kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuanza kufanya kazi Machi Mosi kwa daladala zote zinazotoka na kuingia mjini, kulazimishwa kuingia ndani hata kama sio mwelekeo wake.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wameomba Serikali kuangalia utaratibu mpya kuondoa usumbufu huo.
Wakizungumza na Mwananchi Digital Machi 5, 2025 kwa nyakati tofauti, abiria na madereva wamesema wanapata kadhia hususan wanaotoka Bububu barabara ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Wakati abiria wakitoa kilio hicho, Serikali imekiri kuwapo mzunguko, lakini ikasema hatua hiyo itakuwa ya muda wakati ikiangalia namna ya kuja na usafiri maalumu wa kutoa abiria katika stendi hiyo na kuwapeleke mjini maeneo ya Darajani, Hospitali ya rufaa ya Mnazimmoja na Malindi.
Dereva wa daladala za Bububu, Ramadhan Hussein Haji amesema wanachotaka wao ni kuruhusiwa kutoka Kituo cha Saateni, kwenda Kituo cha Bakhresa na kumalizia Hospitali ya Mnazimmoja kisha wazunguke kupitia Kisonge.
“Abiria wengi wanalalamika kutokana na mzunguko mrefu uliopo kwa sasa hususan kwa daladala za Kidichi, Bububu na Mwanyanya kuanzia Kijangwani na kumalizia Hospitali ya Mnazimmoja,” amesema.
“Kwa sasa mzunguko waliouweka ni mkubwa kwa daladala zinazotoka njia ya Bububu ikiwemo Kijichi, Kwanyanya na Mwanyanya, tunachoiomba Serikali ni kuirudisha ruti ya mwanzo daladala kupitia Kituo cha Bakhresa, Darajani, Mnazimmoja, Tobo la Pili na kumalizia Kijangwani,” amesema.
Abiria wengi wanaotoka upande wa Bububu shughuli zao zipo Malindi na Darajani, hivyo daladala hizo kuanzia Kijangwani ni usumbufu.
Kwa upande wake Yunus Sultan amesema utaratibu wa kutumika kwa kituo hicho sio mzuri, kwani ni usumbufu na inasababisha foleni.
“Kwa daladala zinazotokea upande wa Bububu ni mzunguko na usumbufu, hizo mamlaka haziangalii kuwa katika magari haya ndio tunabeba wagonjwa na wasafiri?.
“Kuna watu watakuja kuachwa na boti kutokana na mzunguko huo, hivyo mamlaka zinazohusika ziangalie upya suala hili,” amesema Yunus
Kila daladala inayoingia katika stendi hiyo inalipia tozo ya Sh1,000 kwa siku.
Sabrina Othman mkazi wa Bububu Ngalawa amesema changamoto ipo hivyo daladala hizo ni vizuri zikatoka Saateni na kuelekea moja kwa moja Bakhresa, Mnazimmoja na kumalizia Kijangwani kama ilivyokuwa awali.
“Daladala kuanzia kituo cha Kijangwani na kumalizia Hospitali kwa kweli ni adha kubwa, tunaoteseka ni wananchi maskini ambao nauli yetu ni moja tu ila kwa hali hiyo wanatutia mashakani kwa sababu lazima tushuke Tobo la Pili na tuchukue usafiri mwingine kuelekea Malindi,” amesema Sabrina.
Naye Mwinyi Mohammed amesema mamlaka zinazohusika zinatakiwa kusimamia maamuzi yake kwa kutoa maelekezo kwa wananchi.
Akijibu malalamiko hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Makame Machano amesema stendi hiyo ndio inakusanya magari yote kama iliyokuwapo darajani kipindi cha nyuma.
Amesisitiza hakuna ruti inayotoka mwanzo wa daladala na kuishia Mnazimmoja, hivyo abiria wanatakiwa kuwa na ustahimilivu hadi wakati utakaopatikana usafiri wa kutoka Kijangwani kuelekea Mnazimmoja, na kutoka Kijangwani kuelekea Malindi bandarini.
“Ufumbuzi wa malalamiko hayo ni kupata usafiri kutoka Kijangwani kuelekea Mnazimmoja na Malindi, kweli tunakiri wanapata usumbufu na hilo tutalifikiria katika kutafuta namna bora,” amesema Makame.
Hata hivyo, amesema njia iliyowekwa na Serikali ambayo itakuja hapo baadaye ni kuwapo kwa usafiri kutoka kituoni hapo kuelekea Mjini.