RC Mara aagiza msako wa wanafunzi wasio ripoti shule

Musoma. Asilimia 17.7 ya wanafunzi waliotakiwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mkoani Mara  kwa mwaka 2025, bado hawajaripoti hadi sasa huku ikielezwa kuwa baadhi yao wamekimbilia nchi jirani wakijihusisha na ajira za utotoni.

Jumla ya wanafunzi 46,671 walipangiwa kujiunga na kidato cha kwanza mkoani Mara kwa mwaka huu,  katika shule zaidi ya 160 za sekondari za umma.

Akifungua kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Mkoa wa Mara (RCC), leo Jumatano Machi 5, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amewaagiza wakuu wa wilaya zote za mkoa huo kuanza msako wa wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni hadi sasa.

“Zipo taarifa kuwa kuna  baadhi ya watoto wapo nchi jirani, wengine migodini wakijihusisha na uchimbaji wa madini hii haikubaliki wote wanatakiwa kuwa shule, wakuu wa wilaya anzeni msako mara moja,” amesema Mtambi

Amesema watoto wengine pia wameshindwa kuripoti shuleni baada ya wazazi wao kuwazuia badala yake kuwataka kufanya  shughuli za uzalishaji mali kama kilimo na kuchunga mifugo.

Mtambi amesema elimu ni haki ya msingi ya mtoto na Serikali haiko tayari kuona yeyote mwenye sifa ya kupata elimu anakosa fursa hiyo kutokana na sababu yoyote ile.

Amesema kesho ya Taifa la Tanzania inawategemea watoto hao, hivyo suala la elimu kwao ni la lazima na mzazi ambaye kwa namna yoyote atasababisha mtoto wake asipate elimu atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Serikali imetoa fedha nyingi sana kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu ili watoto wasome katika mazingira mazuri, hivyo hatuwezi kupepesa macho kwa mzazi atakayekuwa chanzo cha mtoto kukosa elimu kwani atakuwa anacheza na kesho ya Taifa letu,” amesema.

Kuhusu darasa la awali, Mtambi amesema mkoa huo umefanikiwa kuandikisha asilimia 99.61 ya watoto 82,679 waliotarajiwa kuandikishwa kuanza darasa la kwanza hivyo wamevuka lengo kwa asilimia 107, ambapo lengo lilikuwa ni kuandikisha watoto 74,234.

“Hata kama hali ni ngumu hii isiwe sababu ya kumzuia mtoto kwenda shule kwani hii ni kwa faida yake na bahati nzuri sasa hivi kuna elimu bila malipo,” amesema Anna-Rose Joachim.

Joyce Magukura amesema wapo watoto ambao badala ya kwenda shule wazazi wao wamewapeleka maeneo ya mijini kwa ajili ya kufanya kazi za ndani, hali ambayo amesema inavunja haki za mtoto.

“Unakuta mtoto mdogo wa miaka 15 hadi 16 amepelekwa kufanya kazi za ndani umri ambao alitakiwa kuwa shule na kinachoumiza zaidi hata mshahara hapewi yeye anatumiwa mzazi,” amesema.